http://www.swahilihub.com/image/view/-/5022710/medRes/2279283/-/164hkqz/-/mwogeleaji+pic.jpg

 

Muogeleaji Hilal kupewa makali Ugiriki

Muogeleaji nyota wa Tanzania, Hilal Hilal 

Na Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Wednesday, March 13  2019 at  10:09

 

Dar es Salaam. Muogeleaji nyota wa Tanzania, Hilal Hilal amechaguliwa kushiriki kongamano la kimataifa la wanamichezo waliowahi kushiriki mashindano ya Olimpiki Duniani (Woa).

Hilal atashiriki mafunzo maalumu ya ‘International Olympic Academy’s Young Participants Session” yatakayoanza Juni Mosi hadi 15 katika mji Athens, Ugiriki.

Nahodha huyo wa timu ya Taifa ni miongoni mwa wanamichezo wa Tanzania walioshiriki Olimpiki ya Rio 2016 yaliyofanyika katika mji wa Rio De Janeiro, Brazil.

Hilal ni miongoni mwa wanamichezo vijana wawili kati ya 248 duniani waliopata nafasi hiyo akiungana na Sailing, Lijia Xu ambaye ameshiriki Olimpiki ya Beijing China (2008), London Uingereza (2012) na Rio de Janeiro ya 2016.

Hilal ambaye yupo Dubai katika kambi ya mafunzo ya kuogelea chini ya udhaminiwa wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani (Fina) atakapokuwa Ugiriki atajifunza masuala mbalimbali yanayohusiana na michezo ya Olimpiki sanjari na kutembelea eneo ambalo michezo hiyo ilianza.

Mwenyekiti wa Chama Cha Kuogelea Tanzania (TSA) Imani Dominick alimpongeza Hilal kupata nafasi hiyo na alimtaka kuitumia vyema.

“Ni faraja kwa nchi na mchezo wa kuogelea. TSA imefarijika tunaomba Hilal aitumie fursa hiyo kuiletea sifa Tanzania kimataifa,” alisema Dominick.

Muogeleaji huyo alisema atatumia mafunzo hayo kwa masilahi ya nchi na waogeleaji wa timu ya Taifa.