http://www.swahilihub.com/image/view/-/5152706/medRes/2368412/-/ma56wdz/-/rekodi+pic.jpg

 

Mwangata aondoka na rekodi Afrika

Na Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Tuesday, June 11  2019 at  11:21

 

Dar es Saalam. Wadau wa ngumi wamewataka mabondia kufuata nyayo za aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa ya ngumi za ridhaa Benjamini Mwangata.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, nyota wa zamani wa timu ya Taifa walisema rekodi nzuri ya Mwangata katika mchezo wa ngumi inapaswa kuigwa na mabondia nchini.

Mwangata alikutwa amefariki Jumapili asubuhi akiwa nyumbani kwake Gongo la Mboto, Dar es Salaam baada ya majirani kubomoa mlango wa nyumba.

Mwangata aliyezaliwa mwaka 1966 enzi za uhai alishiriki michuano ya Afrika Mashariki katika uzito wa flyweight kwenye michezo miwili ya Olimpiki kuanzia mwaka 1988 mjini Seoul.

Pia Mwangata alicheza michuano ya Jumuiya ya Madola mwaka 1990 na 1998 kabla ya kustaafu na kuwa kocha wa JKT na timu ya Taifa.

Nguli huyo ana rekodi ya kushinda medali ya fedha katika michuano ya Afrika mwaka 1987, baada ya kupoteza pambano la fainali dhidi ya bondia Gemelhu Bezabeh wa Ethiopia aliyeshinda dhahabu.

Akizungumzia rekodi ya Mwangata katika masumbwi, bondia nguli wa zamani, Emmanuel Mlundwa alisema Mwangata alikuwa makini ulingoni na anakumbuka alivyocheza kwa ustadi michuano ya Afrika mwaka 1987 Jijini Nairobi, Kenya.

Mlundwa alisema katika pambano lake la kwanza alimchapa bondia wa Uganda hadi akazimia ulingoni.

"Kwenye ukocha pia alipenda kila bondia aliyepitia mikononi mwake afikie kiwango cha juu, alikuwa mfano wa kuigwa katika ngumi," alisema Mlundwa.

Kauli ya Mlundwa iliungwa mkono na nguli mwingine Andrew Mhoja ambaye alisema atamkumbuka Mwangata kwa ujasiri wake alipokuwa ulingoni kutetea Taifa lake.

"Alikuwa jasiri nakumbuka pambano alilopigana na bondia David Mwamba ambaye alikuwa staa, lakini hakujali umaarufu wa jina lake," alisema Mhoja aliyecheza naye timu ya Taifa.

Alisema Mwangata alipigwa ngumi kali hadi kilinda kichwa (head guard) ikatoka, lakini aliiokota na kuiwahisha kwa kocha wake amvalishe na alirudi haraka ulingoni kuendelea na pambano.

Bondia wa zamani wa uzito wa juu, Koba Kimanga alisema tasnia ya ngumi imepoteza mmoja wa makocha bora ambaye alikuwa makini na mwenye mbinu za ushindi.

Wakati Mwili wa Bondia na kocha wa Timu ya Taifa ya ngumi za Ridhaa,Benjamini Mwangata ukikabidhiwa na polisi jana Jumatatu kwa familia yake kwa ajili ya mazishi, mke wa mwanamasumbwi huyo, Ursula Mwangata amesimulia kifo cha mumewe kilivyowashtua.

Mwangata alikutwa amefariki Juzi Jumapili Asubuhi nyumbani kwake Gongola Mboto Ulongoni, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam baada ya majirani kubomoa mlango wa nyumba yake.

Akizungumza na gazeti hili jana, mke wake Ursula Mwangata alisema Jumatano iliyopita mumewe alikuwa mzima na walikwenda Kibaha kumtembelea mmoja wa vijana wake katika familia.

"Alhamisi alirejea nyumbani na kutuacha sisi kule Kibaha akiwa mzima kabisa, mimi nilibaki kwa kuwa kulikuwa na kikao cha familia Jumamosi, Ijumaa asubuhi alinipigia simu tukazungumza akiwa mzima," alisema mkewe kwa masikitiko.

Alisema licha ya kumtafuta bila mafanikio Jumamosi, majirani walipata wasiwasi kwa kutomuona muda mrefu ndipo walikwenda Serikali ya Mtaa ambapo iliamuliwa kubomoa mlango na kumkuta ndani akiwa amefariki.

"Madaktari baada ya uchunguzi walisema amechelewa kupata msaada, kuna uwezekano alikuwa na tatizo la presha, kifo kimetuachia pigo," alisema Ursula.