Nakumatt FC watafuata mkondo wa maduka yao ligini?

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, October 24  2017 at  21:23

Kwa Muhtasari

VITA vya kukwepa shoka la kuteremka daraja mwishoni mwa kampeni za Ligi Kuu ya KPL mwaka huu vimechacha huku ikisalia michuano minne pekee kwa msimu kutamatika na huenda watakaoteremshwa wakajulikana katika wiki ya mwisho.

 

Limbukeni Nakumatt FC wangali katika hatari ya kushushwa daraja baada ya kupokezwa kichapo cha 1-0 na Bandari.

Wanafainali hao wa Ngao ya GOtv mnamo 2016 kwa sasa wanashikilia nafasi ya 13 kwa alama 35 sawa na Zoo Kericho ambao walibamizwa 1-0 na Posta Rangers ya kocha Sammy 'Pamzo' Omollo.

Mathare United ambao wanatiwa makali na kocha Francis Kimanzi wanashikilia nafasi ya 15 kwa alama 31 sawa na Western Stima ambao walijinyanyua  na kuwakomoa mabingwa wa KPL 2009, Sofapaka kwa mabao 3-1 ugani Narok. 
Chini ya Kimanzi ambaye pia amewahi kuwanoa Tusker na vijana wa Harambee Stars, Mathare United walitawazwa mabingwa wa KPL mnamo 2008.

Ni pengo la alama mbili pekee linalowatenganisha mabingwa hao wa zamani na Thika United ambao kwa sasa wapo katika nafasi ya 17 kwa alama 29.

Ingawa Muhoroni Youth wanakokota nanga mkiani mwa jedwali kwa alama 25, wapo katika uwezekano mkubwa wa kupaa hasa ikizingatiwa kwamba, kwa pamoja na SoNy Sugar, wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na wapinzani wao wakuu.

Wakati uo huo, vita vya kuingia katika kampeni za KPL mnamo 2018 vingali vikali kati ya farasi watano. Ushuru wanajivunia pointi mbili zaidi kuliko KCB nao Vihiga United, Wazito FC na Nairobi Stima wamezoa pointi 65, 62 na 61 mtawalia.

Klabu mbili za kwanza kutoka ligi hii ya timu 19 zitanasa tiketi ya kuingia Ligi Kuu mwaka ujao. Zitachukua nafasi za timu zitakazomaliza kipute cha KPL msimu huu katika nafasi mbili za mwisho. 

Kwa pamoja na KCB, Ushuru FC ambayo iliteremshwa daraja ilipomaliza Ligi Kuu ya 2016 katika nafasi ya 15 kati ya timu 16 zilizoshiriki msimu huo, inaongoza kwa alama 69.

Zikiwa zimesalia mechi tano msimu kumalizika, Ushuru ya kocha Ken Kenyatta imefungua mwanya wa pointi mbili dhidi ya wapinzani wao wa karibu KCB.