http://www.swahilihub.com/image/view/-/5155742/medRes/2370265/-/abuibwz/-/azam+pic.jpg

 

Ndairagije atema cheche Azam

Na Charles Abel, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, June 13  2019 at  12:43

 

Dar es Salaam.Kocha wa Azam Etienne Ndairagije amesema ataendeleza falsafa ya kuwatumia wachezaji vijana katika kikosi chake msimu ujao.

Ndairagije alitoa kauli hiyo jana baada ya kutia saini mkataba wa miaka miwili kuifundisha Azam.

Kocha huyo raia wa Burundi anakwenda kuziba pengo la Mholanzi Hans van der Pluijm aliyetimuliwa katikati ya msimu uliopita kutokana na matokeo yasiyoridhisha.

Ndairagije alisema anapenda kutoa fursa kwa vijana kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo ya soka.

Hata hivyo, alisema hatafumua kikosi cha Azam na anawaamini nyota waliopo watakuwa msada mkubwa katika kutimiza ndoto yake.

Alisema anam furaha kujiunga na Azam moja ya klabu bora katika soka ya ndani na nje.

"Nashukuru uongozi wa Azam kuniamini. Jambo la faraja kwetu kwao kutuamini kwa sababu ni ndoto ambayo tumekuwa nayo ya kuendeleza taaluma yetu,”alisema Ndairagije.

Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin 'Popat' alisema wanaamini kocha huyo atawapa mataji na kuendeleza mfumo wa soka la vijana.

"Kwa niaba ya bodi ya timu, nachukua fursa hii kumkaribisha kocha Etienne. Tumefanya utafiti wa kutosha tukabaini ni mtu sahihi Azam.

“Kipaumbele chetu ni kupata kila kombe tunaloshiriki ndio maana huwa tunafanya vizuri hata kwenye Kombe la Mapinduzi, pia kocha anayetoa fursa kwa vijana," alisema kigogo huyo