Nyangweso ataka Ulinzi wavuruge Al Hilal Benghazi

John Mark Makwatta

John Mark Makwatta wa Ulinzi Stars FC aonyesha tuzo aliyopata ya Mchezaji Bora wa mwezi uwanjani Afraha, Nakuru Mei 19, 2015. Picha/MAKTABA 

Na THOMAS MATIKO na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Friday, February 17  2017 at  17:19

Kwa Mukhtasari

Kocha wa Ulinzi Stars, Benjamin Nyangweso kawaambia vijana wake kuwa lazima 'afe mtu', hivyo atawahitaji watumie kila mbinu kuhakikisha wanazima ‘mchezo mchafu’ wa wapinzani wao Al Hilal Benghazi watakapokutana ugani Kasarani kwenye mechi ya marudio ya kombe la Mashirikisho.

 

KOCHA wa Ulinzi Stars, Benjamin Nyangweso kawaambia vijana wake kuwa lazima 'afe mtu', hivyo atawahitaji watumie kila mbinu kuhakikisha wanazima ‘mchezo mchafu’ wa wapinzani wao Al Hilal Benghazi watakapokutana ugani Kasarani kwenye mechi ya marudio ya kombe la Mashirikisho.

Timu hizi zilichuana Ijumaa  wiki iliyopita jijini Cairo, Misri, Ulinzi wakiwa ugenini kwenye raundi ya kwanza ya mechi za mchujo kuwania taji la Mashirikisho  na leo  jioni wanarudiana. 

Wakiwa huko Uarabuni, vijana wa Nyangweso walilimwa 1-0, ushindi ambao kocha huyo anadai haukuwa halali na uliotokana na mchezo mchafu wa wapinzani wao, huku akitaja bao hilo kuwa la kuotea.

Nyangweso kakemea sana mtindo wa uchezaji wa Al Hilal waliowasili nchini Alhamisi akitahadharisha kuwa wapinzani hao wana mchezo mchafu sana uwanjani hasa upotezaji wakati, mbinu anayosema walitumia sana kwenye mechi yao ya kwanza mara tu baada yao kupata bao ili kuhakikisha wanawazima wanajeshi hao kabisa.

Nyangweso kadai kuwa Al Hilal walipopata lile goli la baada yao kuwapa presha sana ya mapema, walianza kujiangushaangusha kiholelaholela uwanjani na kutafuta fauli zisizokuwa za maana ili wapoteze muda kuhakikisha Tusker hawapati nafasi ya kukomboa.

Hiki ni kitu anachosema anakitarajia kukiona tena leo na ndio maana kawahimiza vijana wake kuwa wabunifu na wajanja wa mbinu zao vile vile zitakazoyeyusha zao Al Hilal.

“Wanacheza kimbuni zaidi. Wanaweza wakaja na kuamua kuifunga mechi kabisa kwa kutofanya mashambulizi yoyote ili kuhakikisha wahatupi mwanya wa kuwapenyeza. Ndio maana nasi lazima tujiaandae. Kikubwa zaidi ni kuhakikisha ngome yetu ya ulinzi ipo makini huku tukipiga hesabu ya namna ya kuwafunga na hapa pia nasi tutahitaji kuwa wajanja,” Nyangweso ametahadharisha.

Nafuu

Nafuu kubwa kwa Nyangweso ni kurejea kikosini kwa mshambuliaji matata Mark Makwatta aliyekosa  mechi ya ugenini kutokana na hitilafu ya pasipoti ambaye anaamini atakuja na ufunguo wa kuwafungua hao Al Hilal kwa kuwa hawakuuona mchezo wake juma lililopita.

Makwatta aliyeifumia Ulinzi jumla ya magoli 28 msimu uliopita ataangaliwa sana kuona ikiwa ataweza kuiondolea fedheha timu ambayo imerejea kwenye soka la kimataifa Barani baada ya kuwa nje tangu 2011 walipobanduliwa na Zamalek wa Misri kwenye raundi ya kwanza ya uwaniaji wa 'Champions League Afrika'.

Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Soka ya Kenya mwaka 2016, John Makwatta ataongoza juhudi za Ulinzi Stars kufufua kampeni yake katika CAF Confederations Cup uwanjani Kasarani, Jumamosi.

Makwata, 24, alikosa mechi ya mkondo wa kwanza Ulinzi ilipolimwa 1-0 na Al-Hilal Benghazi ya Libya iliyochezewa jijini Cairo nchini Misri mnamo Februari 10.

Mshambuliaji huyo, ambaye alipachika mabao 15 msimu 2016 na kumaliza ligi kama mfungaji wa tatu bora msimu 2015 na mabao 14, hakusafiri Misri kwa sababu hakuwa na vyeti vya usafiri.

Vyeti hivyo vilikuwa katika ubalozi wa Uingereza nchini Afrika Kusini kwa shughuli ya kupata visa ya kuelekea nchini Uingereza kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Hull City mnamo Februari 27.

Makwatta ni mmoja wa wachezaji wanaunda timu ya Kenya itakayocheza na Hull uwanjani KCOM.

Katika mahojiano, kocha Benjamin Nyangweso alisema amefurahia kurejea kwa Makwatta kikosini na kuongeza kuwa mchango wake utahitajika sana Ulinzi itakapokuwa ikitafuta kugeuza matokeo ya mkondo wa kwanza.

Wanajeshi wa Ulinzi wanahitaji ushindi wa mabao mawili bila kufungwa ili waweze kuingia raundi ya kwanza. Mshindi wa mechi hii baada ya mikondo miwili atakutana na Smouha ya Misri katika raundi ya kwanza mwezi Machi. Ulinzi itapata tiketi ya kurudi Misri ikibandua nje Benghazi.

Kiingilio cha mechi kati ya Ulinzi na Benghazi uwanjani Kasarani ni Sh100.

Mashabiki wataokaa katika eneo la VIP watalipia Sh300.

Mechi itaanza saa tisa alasiri.

 

Kikosi cha Ulinzi Stars kilichocheza mkondo wa kwanza:

Makipa - James Saruni, Jacktone Odhiambo

Mabeki - Geoffrey Kokoyo, Mohammed Hassan, Benson Sande, Omar Mbongi, Brian Birgen, Sylus Shitote, Hamissi Abdallah Oliver Kiprutto

Viungo - Boniface Onyango, Churchill Muloma, John Kago, Stephen Ochollah, Samuel Onyango, Baron Oketch, Justin Onwong’a

Washambuliaji - Oscar Wamalwa, Evans Amwoka, Enosh Ochieng, Daniel Waweru.