Nzoia Sugar wahemea huduma za chipukizi wa haiba kubwa

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, November 30  2017 at  13:25

Kwa Muhtasari

KATIKA hatua za kujisuka mapema kwa minajili ya kivumbi cha KPL mwaka ujao, kikosi cha Nzoia Sugar tayari kimejinasia huduma za chipukizi Dennis Wafula na Patrick Otieno ambao kwa mujibu wa kocha Bernard Mwalala, watazidisha uthabiti wa idara muhimu kambini mwao. 

 

Wafula ambaye ni mwanafunzi wa shule ya upili ya Misikhu, Bungoma amekuwa akipokezwa malezi ya soka kwa muda mrefu kambini mwa Nzoia ambayo katika msimu wao wa kwanza katika kipute cha KPL mnamo 2017, waliambulia katika nafasi ya tisa jedwalini kwa alama 44.

Otieno ambaye alikuwa pua na mdomo kuingia katika sajili rasmi ya Nzoia kwa mara ya kwanza mnamo Juni 2017 ni mwanafunzi wa shule ya upili ya Bukembe, Bungoma.

Kulingana na Evans Kadenge ambaye ni meneja wa timu ya Nzoia, hatua ya kusajiliwa kwa Otieno na Wafula ni miongoni mwa mikakati kabambe ya kikosi hicho kujifua upya iwapo kitajipata katika ulazima wa kupoteza huduma, ubunifu na maarifa ya nyota Luke Namanda, Brian Otieno, Lawrence Juma na Victor Omondi ambao wanawaniwa pakubwa na klabu maarufu zenye uzoefu mpana katika soka ya humu nchini.