Okumbi hawezi kutimuliwa kazini licha ya matokeo duni, adokeza Mwendwa

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  21:18

Kwa Mukhtasari

RAIS wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa amedokeza uwezekano wa kulifanyia mabadiliko muhimu benchi zima la kiufundi la Harambee Stars baada ya kikosi hicho kupoteza michuano miwili ya kirafiki dhidi ya Iraq na Thailand wiki iliyopita.

 

Ingawa hivyo, Mwendwa amesisitiza kuwa FKF haitampiga kalamu kocha Stanley Okumbi licha ya mashabiki na wadhamini wakuu wa FKF na Ligi Kuu ya KPL, SportPesa kuanza kupoteza imani na mkufunzi huyo wa zamani wa Mathare United na kushinikiza kutimuliwa kwake.

“Shirikisho lina utaratibu wa kufanya kazi. Muhimu zaidi tunalopanga kufanya ni kuandaa kikao cha kutathmini kwa kina utayarifu wa Stars kwa michuano ijayo ya kimataifa. Isitoshe, FKF italenga pia kuzamia baadhi ya changamoto zinazokabili timu ya taifa kiasi cha kuchangia kushuka kwa kiwango cha ubora wa kikosi kizima,” alitanguliza kinara huyo.

“Hatuwezi kumfuta kazi Okumbi kutokana na presha ya kijisehemu ya mashabiki ambao wanasisitiza ulazima wa kutimuliwa kwa kocha huyo. Itakuwa vyema kuzungumza mwanzo na wachezaji pamoja na benchi la kiufundi ili kubaini kilichojiri katika michuano iliyowakutanisha na Iraq na Thailand,” akaongeza kinara huyo.

Kwa mujibu wa Mwendwa, timu ya taifa inazidi kukomaa na kuimarika zaidi chini ya ukufunzi wa Okumbi, kocha ambaye Afisa Mkuu Mtendaji wa Sportpesa, Ronald Karauri amesisitiza hana ujuzi wa kunoa timu ya taifa.

Okumbi ni mwingi wa matumaini kwamba Stars watajinyanyua katika mapambano yajayo ya kimataifa, hasa katika kivumbi kitakachowakutanisha na Ghana katika juhudi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) za 2019 nchini Cameroon.

Licha ya Stars kusajili sare ya 1-1 dhidi ya Msumbiji na Mauritania kisha kupokezwa kichapo cha 2-1 na 1-0 kutoka kwa Iraq na Thailand mtawalia, Mwendwa amesisitiza kuwa timu ya taifa ina uwezo wa kurejelea makali yake ya awali na kutikisa zaidi ngome za baadhi ya vikosi maarufu katika siku za usoni iwapo timu itashirikishwa katika michuano mingi zaidi ya kupimana nguvu.