Olunga alishwa benchi Girona ikipiga Coruna 2-1

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Tuesday, October 24  2017 at  20:36

Kwa Muhtasari

GIRONA anayochezea Mkenya Michael Olunga ilipata ushindi wake wa pili katika Ligi Kuu ya Uhispania (LaLiga) kwa kulima wenyeji Deportivo La Coruna 2-1 Jumatatu.  

 

Klabu hii, ambayo iliingia Ligi Kuu kwa mara ya kwanza katika historia yake msimu huu wa 2017/2018, ilivuna ushindi kupitia penalti ya Aday iliyopatikana dakika ya 25 na Portu dakika ya 71. Mvamizi wa zamani wa Arsenal, Lucas Perez, alipachika bao la Deportivo kupitia penalti dakika ya 51.

Girona haikuwa na ushindi kwenye ligi katika mechi sita kabla ya kuzima Deportivo. Ushindi wake wa kwanza katika Lugi Kuu ulikuwa 1-0 dhidi ya Malaga mnamo Agosti 26.

Baada ya mechi hii, ambayo Olunga alikuwa shabiki tu kwenye benchi, Girona imeruka nafasi moja juu na kutua nambari 15. Imezoa pointi tisa kutoka mechi tisa.

Deportivo imeteremka nafasi moja hadi nambari 16. Ina jumla ya pointi nane katika ligi hii ya klabu 20. Barcelona inaongoza jedwali kwa alama 25.

Inafuatwa na Valencia (21), mabingwa watetezi Real Madrid (20), Atletico Madrid (19), Leganes (17) nazo Villarreal, Real Betis na Sevilla zimezoa pointi 16 kila mmoja. Kwingineko katika Ligi Kuu ya Norway, wenyeji Odd walipepeta Lillestrom anayochezea Kipa Mkenya Arnold Origi 1-0 kupitia bao la Sigurd Haugen, Jumatatu. 

Kichapo hiki cha nne katika mikojo ya Odd kinafanya Lillestrom isalie katika nafasi ya 11 katika ligi hii ya klabu 16 kwa alama 31 kutoka mechi 26. Odd inashikilia nafasi ya saba kwa alama 38.