Olunga awazia kurejea Uchina licha ya kumezewa mate na CSKA Moscow

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, October 24  2017 at  13:02

Kwa Muhtasari

KIKOSI cha Guizhou Zhicheng ambacho ni mwajiri rasmi wa nyota wa zamani wa Gor Mahia, Michael Olunga kimejipa uhakika wa kushiriki kipute cha Ligi Kuu ya China msimu ujao wa 2018 licha ya kubamizwa 5-1 na mabingwa watetezi,  Guangzhou Evergrande.

 

Zikisalia mechi mbili pekee kwa jamvi la Ligi Kuu ya China kukunjwa rasmi msimu huu, kocha Gregorio Manzano amewachochea Guizhou kutinga mduara wa saba-bora kwa alama 39 japo pengo la pointi 25 linatamalaki kati yao na viongozi  Guangzhou.

Ujio wa Manzano kambini mwa Zhicheng ni moja kati ya sababu zilizomchochea Olunga kutumwa kwa mkopo hadi Girona FC ya Uhispania msimu huu baada ya mkufunzi huyo kumweka fowadi huyo wa Harambee Stars nje ya mipango ya Zhicheng ambao walipandishwa daraja msimu uliopita.

Ingawa hivyo, huenda Olunga akalazimika kurejea China kuwasakatia waajiri wake hao msimu ujao au akahiari kutafuta hifadhi kwingineko hasa ikizingatiwa hatua ya hivi majuzi ya Catalonia kutaka kujiondoa kutoka Uhispania na kuwa taifa huru.

Japo anahusishwa pakubwa na Osmanlispor ya Uturuki, Olunga amedokeza kwamba anawaniwa pia na CSKA Moscow (Urusi), Galatasaray (Uturuki), Olympique Lyon (Ufaransa) na Real Betis (Uhispania). 

Kikosi cha Beijing Renhe ambacho pia kinampa hifadhi nyota wa Kenya, Ayub Masika nchini China tayari kina uhakika wa kunogesha kampeni za Ligi Kuu msimu ujao baada ya kupandishwa ngazi kutoka Ligi ya Daraja la Pili.