http://www.swahilihub.com/image/view/-/4924434/medRes/2217354/-/tecm3i/-/kingara.jpg

 

RYSA FC yatwaa Simon King'ara CDF Cup

Simon King'ara

Mbunge wa Ruiru Simon King'ara (wa tatu kulia na suruali fupi ya manjano) akikabidhi timu ya RYSA FC taji la King'ara CDF Cup baada ya vijana hao kupata ushindi Jumapili, Januari 6, 2018, katika uwanja wa Ruiru. Picha/LAWRENCE ONGARO 

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Monday, January 7  2019 at  11:55

Kwa Muhtasari

RYSA FC ya Ruiru ndiyo mabingwa wa Simon King'ara CDF Cup.

 

RUIRU, Kenya

VIJANA wa Kassa FC waliona moto wa jiwe mbele ya RYSA FC ya Ruiru, walipopokezwa kichapo cha mabao 5-1 kwenye fainali ya kuwania taji la Simon King'ara CDF Cup, iliyoandaliwa Jumapili katika uwanja wa Ruiru.

Katika pambano hilo lilishuhudiwa na mashabiki wapenda kandanda, RYSA ilitangulia kutia kimiani bao la kwanza kupitia juhudi zake Martin Mwangi dakika ya 10 ya mchezo.

Vijana wa RYSA walizidisha mashambulizi yao makali kwenye eneo la wapinzani na kwa mara nyingine mvamizi matata Martin Mwangi, alifuma kimiani bao la pili dakika ya 25.

Kipindi cha lala salama, mambo yalizidi kuwa magumu kwa vijana wa Kassa, ambapo ngome yao ilivamiwa bila huruma.

Katika dakika ya 50, Simon Mbugua alifanya kweli na kufunga bao la tatu.

Lakini vijana wa Kassa hawakutaka kutoka mikono mitupu uwanjani, na katika dakika ya 62 Isaac Okaka mshambulizi matata alijipenyeza kati ya madifenda wawili na kuzititiga nyavu.

Washindi walifunga ukurasa na bao la tano kupitia straika matata Hector Bunde kunako dakika ya 84.

Vijana wa RYSA walipokea kikombe, jezi, mpira na Sh30,000.

Kassa FC nayo kwenye nafasi ya pili ilijivunia jezi, mpira na Sh25,000. Timu ya CCIC (County Community), ilipokea Jezi mpira na Sh20,000.

Halafu Mwihoko FC ya nne iliridhika na Sh15,000.

Mfadhili wa mashindano hayo ambaye ndiye Mbunge wa Ruiru, alisema mashindano hayo yatakuwa yakiendeshwa kila mara ili kuleta utangamano miongoni mwa vijana na wakazi wa Ruiru kwa jumla.

"Nitazindua pia michezo ya wasichana katika michezo ya soka na Netiboli ili nao wajisikie kama wenzao wavulana," alisema Kinga'ara.

Kocha Gilbert Liyai wa RYSA alitambuliwa kama mkufunzi stadi na kupokea medali. Naye refarii Henry Gitau aliyechezesha mechi hiyo pia alitambuliwa kama mwamuzi wa kutegemewa na kutunukiwa medali.