Rachier amtaka Ze Maria kumtajia udhaifu wa Gor Mahia

Na THOMAS MATIKO

Imepakiwa - Friday, February 17  2017 at  15:32

Kwa Mukhtasari

Kocha wa Gor Mahia, raia wa Brazil Ze Maria, kwa sasa ni sawa na mtu aliyekalia kuti kavu.

 

KOCHA wa Gor Mahia, raia wa Brazil Ze Maria, kwa sasa ni sawa na mtu aliyekalia kuti kavu.

Hata kabla ligi kuu ya msimu huu haijaanza kutokana na mzozo unaendelea kati ya FKF na KPL, mashabiki wa K'Ogalo tayari wameanza kumshinikiza mwenyekiti wao Ambrose Rachier afanyie mabadiliko benchi ya ukufunzi.

Unajua ni kwa nini? 

Licha ya Ze Maria kuwaongoza Gor kumaliza wa pili ligini msimu uliopita mashabiki hao hawajaridhishwa kabisa na maandalizi yake ya timu kwa ajili ya msimu mpya.

Hadi kufikia sasa, Gor wamecheza mechi nne za kirafiki ya kujipima nguvu kwenye programu yao ya maandalizi na kupoteza zote.

Kwa mechi yao ya kwanza ya kujipima nguvu, walisafiri hadi Sudan kuchuana na miamba wa huko Al Hila Omdurman na kulimwa 1-0.

Wiki moja baadaye wakapimana nguvu na Thika United ugani Camp Toyoyo na kulimwa 2-1. Baadaye walisafiri hadi Uganda na kukipiga dhidi ya Onduparaka na kulimwa 2-0  na hivi majuzi Jumatano, wakalambwa na limbukeni Administration Police wanaoshiriki divisheni ya  pili 3-2.

Ni matokeo ambayo tayari yameshawaingiza mkenge  mashabiki wa Gor ambao sasa baadhi yao wanamshinikiza Rachier akifanyie mabadiliko benchi ya ukufunzi, mapema kabla msimu haujaanza ili kuepuka fedheha hapo baadaye.

Mwenyekiti Rachier kaungama kuwepo na shinikizo hilo kutoka kwa mashabiki wanaompiga simu na wengine wakimtumia ujumbe ila kaamua kumkingia Ze Maria na kusema hana mpango wa kumtimua  huku akiwataka mashabiki wawe na subra naye.

Shida

Rachier anasema amezungumza na Ze Maria kutaka kufahamu ni nini tatizo na maweza kumridhisha na majibu yake na ndio maana kaafiki ni vyema kumvumilia muda zaidi. Hata hivyoligi ikianza , mechi tatu za kwanza   ndizo huenda zikaamua hatma yake kwa mujibu wa watu wa karibu wa vinara wa klabu hiyo.

“Nilimwita kocha na kuzungumza naye nikitaka kujua kulikoni na akanipa majibu ya kuridhisha mbona tumepoteza mechi zile. Kule Sudan alisema kikosi kilikuwa ndio mwanzo kimetoka likizoni hivyo akili zao hazikuwa zimetulia na isitoshe hawakuwa na muda wa kutosha kufanya mazoezi mazuri. Dhidi ya Thika alisema alikipanga kikosi chenye asilimia kubwa ya sajili wapya ili kutaka kumsoma kila mchezaji mpya na tulipokutana na Onduparka anasema kikosi hakikuwa fiti kabisa,” akafunguka.

Kiongozi huyo kasisitiza kuwa hawezi kumtimua kocha kwa matokeo ya mechi za ‘Pre-season’ kwa sababu sio njia mwafaka ya kupima uwezo wa kocha na kushikilia kuwa kama akifanya hivyo, atakuwa kaanzisha mtindo mbaya.

“Ni vyema mwanzo kuketi na kocha na kufahamu tatizo lipo wapi ma itakuwa ni kuanzisha mtindo mbaya kama tukimfurusha kutokana na matokeo mabovu ya maandalizi ya msimu mpya wakati tumempa malengo anayotakiwa kufanikisha msimu utakapoanza,” Rachier akaongeza.