Raundi hii ni mlima kuetetea ubingwa, akiri Nsibe

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  21:15

Kwa Mukhtasari

KOCHA George ‘Best’ Nsimbe wa Tusker amekiri kwamba huu ndio msimu mbaya zaidi anaoushuhudia katika kipindi cha taaluma yake ya ukufunzi.

 

Isitoshe, ameungama kusalimu amri katika juhudi za kufukuzia ubingwa wa KPL msimu huu kwa kudokeza ugumu wa kuwafikia Gor Mahia kileleni mwa jedwali.

Baada ya Tusker kulazimishiwa sare tasa na Kariobangi Sharks katika mechi ya KPL iliyowakutanisha uwanjani Ruaraka mnamo Oktoba 12, 2017, vijana wa Nsimbe ambaye aliaminiwa kudhibiti mikoba aliyoachiwa na kocha Paul Nkata mwishoni mwa msimu jana wanasalia katika nafasi ya saba kwa alama 40 sawa na Posta Rangers ya mkufunzi Sammy ‘Pamzo’ Omollo.

Hadi kupokezwa mikoba ya Tusker ambao ni washindi mara 11 wa taji la KPL, Nsimbe alikuwa akiwatia makali vijana wa KCCA, mabingwa mara tatu wa ligi kuu ya soka Uganda ambao walipepetana na Tusker kirafiki mwanzoni mwa Januari 2017. Isitoshe, mkufunzi huyo alikuwa amedhibiti kwa kipindi kirefu mikoba ya klabu mbalimbali zinazoshiriki soka ya Tanzania.

Sare tasa dhidi ya Sharks ni matokeo ambayo Nsimbe amesisitiza yalididmiza zaidi matumaini finyu waliokuwa nayo ya kutetea kwa mafanikio ubingwa wa KPL mwaka huu.

Sharks ambao walipandishwa ngazi kushiriki kipute cha KPL mwishoni mwa msimu jana kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano jedwalini kwa alama 41, nne nyuma ya Sofapaka na Kakamega Homeboyz ambao wanashikilia nafasi za pili na tatu mtawalia.

Mabingwa mara nne, Ulinzi Stars wanafunga mduara wa nne-bora kwa alama 42, mbili zaidi kuliko Posta Rangers na Tusker ambao pia walitia kapuni ubingwa wa KPL Top8 mwishoni mwa msimu uliopita.

Iwapo Gor Mahia wataendeleza ubabe wao na kusajili ushindi katika jumla ya michuano mitatu ijayo basi watakuwa wakitawazwa wafalme wa taji hilo kwa mara ya 16, miaka miwili baada ya kujinyakulia ubingwa wa Ligi Kuu bila ya kupoteza mchuano wowote.

Ufahamu wa wepesi uliopo mbele yao na ukubwa wa matarajio kutoka kwa mashabiki ni jambo ambalo limemchochea kocha Dylan Kerr kuwahimiza vijana wake kutotepetea katika michuano iliyopo mbele yao na kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kutawazwa mabingwa wa KPL msimu huu.