Ruto na Chumba wadaka mkwanja Beirut Marathon

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Sunday, November 12  2017 at  14:49

Kwa Muhtasari

MKENYA Dominic Ruto na Mbahraini Eunice Chumba wametia kibindoni Sh1, 346, 800 kila mmoja baada ya kunyakua mataji ya Beirut Marathon nchini Lebanon, Jumapili.

 

Ruto na mzawa wa Kenya, Chumba, walijishindia Sh1,036,000 kwa kushinda taji na kuongezwa bonasi ya Sh310,800 kwa kufuta rekodi za Mkenya Jackson Limo (2:11:04) na Muethiopia Muhalbat Tsege (2:29:12) zilizokuwa zimedumu tangu mwaka 2015 na 2014, mtawalia.

Ruto alivunjilia mbali rekodi ya Limo kwa kutimka umbali huo wa kilomita 42 kwa saa 2:10:41 naye Chumba alikata utepe kwa saa 2:28:38.

Mabingwa wa mwaka 2016 Edwin Kiptoo (Kenya) na Tigist Girma (Ethiopia) walishindwa kutetea mataji yao. Walizawadiwa Sh362, 600 na Sh621, 600 baada ya kukamilisha mbio katika nafasi ya tatu na mbili, mtawalia. Makala haya ya 15 yalivutia washiriki 47,800.  

 

Matokeo ya Beirut Marathon (Novemba 12):

Wanaume

Dominic Ruto (Kenya) saa 2:10:41

Adane Amsalu (Ethiopia) 2:10:45

Edwin Kiptoo (Kenya) 2:11:56

 

Wanawake

Eunice Chumba (Bahrain) 2:28:38

Tigist Girma (Ethiopia) 2:29:00

Debebe Getachew (Ethiopia) 2:30:31