Salah awapiku Aubemeyang, Mane Afrika

Mohamed Salah 

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  08:37

Kwa Muhtasari

Ametangazwa mchezaji bora wa Afrika 2018.

 

Dakar, Senegal. Mshambuliaji wa Liverpool na Misri, Mohamed Salah ametangazwa mchezaji bora wa Afrika 2018. Salah ametwaa tuzo hiyo katika hafla iliyohudhuriwa na watu mashuhuri akiwemo Rais wa Liberia George Weah.

Mshambuliaji huyo amepata mafanikio hayo baada ya kufunga mabao 32 ya Ligi Kuu England na 44 katika mashindano yote msimu 2017/2018.

Nyota huyo alifunga mabao mawili katika fainali za Kombe la Dunia ambazo Misri ilishiriki kwa mara ya kwanza, baada ya kupita miaka 28.

Pia nahodha huyo wa Misri mwenye miaka 26, aliisaidia Liverpool kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Mei, mwaka jana.

Salah aliibuka kinara katika hafla iliyofanyika juzi usiku mjini Dakar, Senegal ambapo alimpiku mchezaji mwenzake Sadio Mane na nyota wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang.

Muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi, Salah aliyetwaa tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo, alipanda jukwaani na kucheza muziki.

Salah alipata kura nyingi zilizopigwa na wakurugenzi wa benchi la ufundi na makocha kutoka nchi 56, mwanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kikosi bora Afrika kinaundwa na Salah, Mane, Aubemeyang, Naby Keita, Riyad Mahrez, Eric Bailly , Serge Aurier, Medhi Benatia, Kalidou Koulibaly, Thomas Partey na kipa Denis Onyango.