http://www.swahilihub.com/image/view/-/3394922/medRes/1444937/-/114js0b/-/golimalia.jpg

 

Sare ya Gor Mahia dhidi ya Sofapaka yatishia hesabu yao

Karim Nizigimana

Karim Nizigimana (kushoto) wa Gor Mahia awania mpira dhidi ya Jaffar Gichuki wa Sofapaka uwanjani Nyayo Septemba 25, 2016. Picha/MARTIN MUKANGU 

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, September 26  2016 at  08:36

Kwa Muhtasari

Gor Mahia walipata pigo kubwa katika kampeni yao ya kushinda Ligi Kuu ya Soka ya Kenya kwa mwaka wanne mfululizo baada ya kukabwa 0-0 na wavuta-mkia Sofapaka uwanjani Nyayo, Jumapili.

 

GOR Mahia walipata pigo kubwa katika kampeni yao ya kushinda Ligi Kuu ya Soka ya Kenya kwa mwaka wanne mfululizo baada ya kukabwa 0-0 na wavuta-mkia Sofapaka uwanjani Nyayo, Jumapili.

Zikiwa zimesalia mechi tano msimu 2016 umalizike, Gor wako pointi nne nyuma ya viongozi Tusker, ambao waliingia raundi ya mechi za 25 wakiwa pointi mbili pekee mbele ya mabingwa hawa mara 15 wa Kenya.

Nayo Thika United iliponea kupoteza mechi yake ya tatu mfululizo dhidi ya SoNy Sugar baada ya kupata bao la kuchelewa katika sare ya 1-1.

Victor Ademba alipatia SoNy uongozi dakika ya 26, lakini Thika ikajibu kupitia Saad Musa zikisalia dakika 13 mechi kumalizika.

Kabla ya sare hii, SoNy ilikuwa imezamisha Thika 1-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza mwezi Mei na kuwika tena 2-0 katika awamu ya lala-salama ya mwaka 2015. Mara ya mwisho Thika ilipiga SoNy katika ligi ilikuwa katika mechi ya mkondo wa kwanza 2015.

Ilishinda 1-0 ugenini.

Thika imepata pointi tatu pekee kutoka mechi zake tano za mwisho nayo SoNy imevuna pointi nane kutoka idadi sawa ya mechi.

Katika mechi iliyofungua siku, Mathare United na Posta Rangers zilitoka sare kwa mara ya sita mfululizo. Klabu hizi zilimaliza mechi bila kufungana kama zilivyofanya katika mechi ya mkondo wa kwanza mwezi Mei na msimu 2011.

Msimu 2012, klabu hizi zilitoka sare ya 1-1 nyumbani na ugenini. Rangers ilitemwa mwisho wa msimu huo kabla ya kurudi Ligi Kuu msimu huu.

Hatari ya kutemwa

City Stars, ambayo ilipiga Bandari 3-1 Jumamosi, na Sofapaka ziko ndani ya mduara hatari wa kutemwa.

City inakamata nafasi ya 15 na pointi 17 nayo Sofapaka imezoa pointi 16. Nambari 14 Ushuru iko pointi saba nje ya mduara huu wa kutupwa hadi ligi ya daraja ya pili.

Matokeo ya mechi za raundi ya 25:

Septemba 23 – Tusker 2 Muhoroni Youth 1; Septemba 24 – Bandari 1 Nairobi City Stars 3, Kakamega Homeboyz 1 Ushuru 1, AFC Leopards 0 Western Stima 1, Chemelil Sugar 1 Ulinzi Stars 0; Septemba 25 – Mathare United 0 Posta Rangers 0, Thika United 1 SoNy Sugar 1, Gor Mahia 0 Sofapaka 0