http://www.swahilihub.com/image/view/-/5134500/medRes/2356457/-/oddcr7z/-/savio+pic.jpg

 

Savio yajifariji kuboronga RBA

Na Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Tuesday, May 28  2019 at  09:56

 

Dar es Salaam.Baada ya kupoteza mechi sita katika Ligi ya Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (RBA), kocha wa Savio, Evarist Mapunda amesema bado wana nafasi ya kufanya vyema kwenye michuano hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mapunda alisema mkakati wa Savio ni kutetea ubingwa wa RBA msimu huu licha ya kuanza vibaya ligi hiyo.

Savio imecheza mechi 11 na kufungwa sita huku mmoja ukiwa ni ule na Oilers ambapo timu hiyo ilikacha Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam.

"Huu ni upepo tu ambao tunaamini unavuma na kutulia, tutakaa sawa na tutaendeleza rekodi yetu," alisema kocha huyo mwenye historia ya kuipa Savio mataji ya RBA misimu mitatu mfululizo.

Savio ni ya nane katika msimamo ikiwa na pointi 15 huku washindani wao, Oilers ikikalia usukani kwa pointi 22 katika michezo 12 iliyocheza na kushinda 11.

Maafande wa JKT wameshushwa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo, lakini imezidiwa mchezo mmoja na Oilers katika Ligi hiyo.

Mpaka sasa JKT ndiyo timu pekee ambayo haijafungwa kwenye RBA msimu huu ikiwa na pointi 22 katika michezo 11 iliyocheza na imesalia na michezo minne kumaliza mechi za mzunguko wa kwanza.

&&&&&&&

Mtemi ampa ushauri Amunike kuisuka Stars

Imani Makongoro, Mwananchi

imakongoro@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.Nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Mtemi Ramadhani amemshauri Kocha Emmanuel Amunike kujenga stamina ya wachezaji.

Taifa Stars itashiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) zilizopangwa kuanza Juni 19 hadi Julai 21 nchini Misri.

Akizungumza jana, Mtemi alisema Taifa Stars inapaswa kutengeneza stamina ya kutosha ili kushindana na wachezaji wa nchi nyingine.

"Pamoja na kutengenezwa stamina, Taifa Stars  inatakiwa kucheza mechi kadhaa za kirafiki ili kujiweka fiti," alisema kiungo huyo nguli.

Taifa Stars imepangwa Kundi C na timu za Kenya, Senegal na Algeria. Timu 24 zinatarajiwa kushiriki fainali hizo.

Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco alisema Taifa Stars inatarajiwa kuanza kambi Mei 30.

Morocco alisema kambi itaanza Dar es Salaam kabla ya kwenda nje ya nchi na timu hiyo itacheza mechi mbili za kimataifa za kirafiki kabla ya mashindano ya Afcon.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania Tanzania (TFF), Wallace Karia alisema timu hiyo itakwenda kuweka kambi Misri ingawa hakuweka wazi lini timu hiyo itaanza mazoezi kujiandaa kujiandaa kwa AFCON.