Shinikizo zachacha kutaka ushuru wa kamari upunguzwe

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Friday, April 21  2017 at  06:41

Kwa Mukhtasari

SHINIKIZO linazidi kupanda kuhusu pendekezo la serikali ya Kenya kutaka kuongeza ushuru inazotoza kampuni za bahati nasibu kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 50.

 

Kampuni ya hivi punde kuongeza sauti yake ikitaka pendekezo hilo kuangaliwa upya ni ile inayoendesha Ligi Kuu ya Soka ya Kenya (KPL).

Imesema kuwa ushuru huo utaua kampuni za bahati nasibu na sekta ya spoti na kuongeza kuwa serikali haitaweza kufadhili spoti kupitia mradi wake kitaifa bila ya mchango kutoka kwa kampuni hizo za bahati nasibu.

Katika taarifa yake Alhamisi, KPL imeitaka serikali kuangalia upya pendekezo hilo lililotangazwa na Waziri wa Hazina ya Kitaifa, Henry Rotich katika bajeti yake mnamo Machi 30, 2017.

“Ligi Kuu ya Soka ya Kenya ni mojawapo ya mashirika mengi nchini yanayonufaika na udhamini kutoka kwa kampuni za bahati nasibu. Kampuni hizi zikikumbwa na matatizo na kukosa kufikia malengo yao, basi zitalazimika kukatiza ufadhili wao kwa mashirika ya kispoti na kuathiri vibaya michezo.

“Mbali na Ligi Kuu, klabu nne zinazoshiriki ligi hii AFC Leopards, Gor Mahia, Mathare United na Sofapaka zinadhaminiwa na kampuni za bahati nasibu na kupitia udhamini huo, ligi na klabu hizi zimeweza kugharamia shughuli zao,” ilisema taarifa hiyo kutoka kwa Afisa Mkuu Mtendaji Jack Oguda.  

Aliongeza, “Kupitia ufadhili huo, klabu zimeweza kulipia gharama za siku ya mechi kama vile kukodisha viwanja vinavyo milikiwa na serikali, ambulanzi, maafisa wa polisi, watoto wa kuleta mipira, kampuni za tiketi pamoja na kampuni za kutangaza mechi, gharama za usafiri na kulipa mahala pa kulala, na kadhalika) pamoja na kulipa mishahara ya wachezaji, maafisa wa benchi la kiufundi, marefa, walinzi, wasimamizi wa mechi na maafisa wengine wanaohusika katika shughuli za siku ya mechi kwa njia moja ama nyingine."

Kutoka orodha hiyo ni wazi kuwa sekta nyingi zinazonufaika na sekta nzuri ya spoti zinategemea ufanisi na ukuaji wa kampuni za bahati nasibu.

“Kuanguka kwa kampuni za bahati nasibu kwa hivyo hakutaua sekta ya spoti tu, bali pia sekta zingine zinazopata mapto kutoka kwa spoti.

Mafanikio tunayoshuhudia katika sekta ya spoti yanatokana na udhamini wa kampuni za bahati nasibu na kwa hivyo yataathirika vibaya sana kiasi kuwa haitakuwa rahisi kuyapata kupitia mradi wa kitaifa wa spoti, utamaduni na sanaa.

KPL itaunga mkono miradi ya serikali inayolenga kuimarisha sekta ya spoti, lakini ni wazi kuwa mradi wa kusaidia sekta ya spoti kupitia serikali hautafanikiwa kwa sababu mapato yake yanatoka katika kampuni za bahati nasibu,” taarifa ya KPL ilisema.

Mashirikisho yanayosimamia raga nchini (KRU) na soka (FKF), kampuni ya Bradley Limited inayoendesha michezo ya bahati nasibu ya SportPesa na Pambazuka National Lottery ni baadhi ya mashirika yaliyolalamika kuhusu ushuru kuongezwa.

SportPesa inadhamini KRU na timu za taifa za raga za watu wazima kwa karibu Sh607 milioni na klabu za Gor Mahia na AFC Leopards kwa karibu Sh50 milioni, huku kampuni za bahati nasibu za Betika na Betway zikidhamini Sofapaka na Mathare United, mtawalia.