http://www.swahilihub.com/image/view/-/4919386/medRes/2213993/-/3e13fv/-/chuana.jpg

 

Shughuli iko leo Etihad, dakika 90 zitaamua

Awali, Manchester City walipokuwa wakichuana na  Liverpool 

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Thursday, January 3  2019 at  08:53

Kwa Muhtasari

Liverpool ipo nafasi ya kwanza, pointi 54 na City ya pili ikiwa na pointi 47

 

MANCHESTER, England. Hoja inayokuja mbele ni kwamba, fundi wa kuzichanga karata, ndiye atakayeibuka mshindi katika pambano la leo usiku kwenye Uwanja wa Etihad wakati Manchester City itakapokuwa mwenyeji wa Liverpool, mechi ya Ligi Kuu England.

Mpambano huo uliokuwa gumzo tangu mwishoni mwa mwaka jana, una mambo makubwa mawili, ama Liverpool kuendeleza ubabe wake kwa Manchester City au Manchester City kumaliza mbio za Liverpool kucheza mechi 21 bila kupoteza mechi ya Ligi Kuu.

Mpaka sasa Liverpool iko kwenye nafasi ya kwanza ikiwa na pointi zake 54 baada ya mechi 20 wakati City iko nafasi ya pili ikiwa na pointi 47. Ushindi wa City utapunguza wigo wa pointi na kubakisha nne na endapo Liverpool itashinda itatanua wigo na kufikisha pointi 57.

Hata hivyo, katika mchezo huo, Ilkay Gundogan anatarajia kurejea kikosini Manchester City baada ya kukosa mechi ya Southampton kutokana na kuwa majeruhi wakati salama ya Liverpool ni kukosekana kwa Kevin De Bruyne anayesumbuliwa na misuli.

Mwingine ambaye atakosa mechi hiyo ni Fabian Delph ambaye amesimamishwa wakati Benjamin Mendy ni majeruhi wa muda mrefu.

Liverpool nayo, kiungo wake, James Milner amepona msuli uliomweka nje kwa muda sasa huku Alberto Moreno aliyekuwa na nyama za paja amepona. Jordan Henderson na Naby Keita wote wako sawasawa.

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola alisema: “Liverpool ni moja ya timu bora Ulaya hata duniani kwa sasa.

“Hilo halina ubishi. Tutakachofanya ni kupambana, kufanya kazi yetu, tutaingia uwanjani, tutapambana na mwisho wa siku tutaona.”

Kocha huyo ana kazi moja, kulipa kisasi cha kupoteza mechi zote mbili za Ligi Kuu msimu uliopita kwani pamoja na City kutwaa ubingwa wa EPL, Liverpool iliwapiga nje ndani.

Akizungumzia upande wake, kocha wa Liverpool, Jürgen Klopp alisema: “Tulipokwenda nyumbani kwa Manchester City mwaka jana, tuliwapiga kwao hukohuko, wao walikuwa wanaongoza, sisi tulikuwa wanne. Kwa hilo hatuna wasiwasi nalo.

“Tunawafuata City na tutawapiga ili tuwaache mbali, tunakwenda pale kucheza mpira wetu na ninaamini tutafanikiwa kwa asilimia 100.

“Wakati tunaanza msimu, tulikuwa tunawaza kama tutaweza kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya na tulikuwa na wasiwasi na City lakini hawajaonyesha kutisha msimu huu.

“Sasa tumewaacha mbali kiasi japokuwa bado kuna kitu cha kufanya zaidi.”