http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119294/medRes/1996762/-/gc1ckwz/-/pointi+pic.jpg

 

Simba bado pointi tano

Na Thomas Ng’itu, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  09:27

 

Dar es Salaam. Simba imebakiza pointi tano kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya jana kuichapa Mtibwa Sugar mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Pia matokeo ya jana yameirudisha Simba katika usukani wa ligi baada ya kufikisha pointi 85 na kuiporomosha Yanga hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi 83.

Endapo Simba itashinda mechi mbili au moja na kutoka sare mechi mbili kati ya nne zilizobaki dhidi ya Singida United, Ndanda, Biashara United na Mtibwa itafikisha pointi 91 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.

Yanga iliyobakiwa na mechi mbili dhidi ya Mbeya City kabla ya kumaliza na Azam, kama itashinda michezo yote miwili itafikisha pointi 89 ambazo tayari zitakuwa zimepitwa na Simba.

Ushindi wa Simba umeendeleza rekodi nzuri dhidi ya Mtibwa katika mechi 11 za Ligi Kuu ambapo imeifunga mechi saba na sare nne katika misimu mitano zilipokutana.

Mtibwa ina rekodi ya kufunga mabao matatu katika mechi 11, imefungwa mabao 14 na haijaifunga Simba kwa miaka sita tangu iliposhinda 2-0 Februari 24, 2013.

Hesabu sahihi za benchi lake la ufundi zilizochagizwa na makosa ya kiufundi ya Mtibwa, zilichangia Simba kupata pointi tatu.

Kocha Patrick Aussems alijilipua kwa kujaza idadi kubwa ya wachezaji wenye asili ya kushambulia hadi kwenye benchi, mbinu iliyozaa matunda kwa kuinyima uhuru safu ya ulinzi ya Mtibwa iliyokuwa ikifanya makosa mara kwa mara.

Tofauti na Simba iliyoanza na viungo watatu, Mtibwa ilianza na wawili ambao ni nahodha Shabani Nditi na Ally Makarani ambaye kiasili ni mshambuliaji wa pembeni huku ikianza na washambuliaji wanne Salum Kihimbwa, Riphat Khamis, Haruna Chanongo na Jaffari Kibaya.

Mchezo ulivyokuwa

Simba ilianza kwa kasi mchezo na ilifanya mashambulizi langoni mwa Mtibwa dakika ya saba na 18 kupitia kwa Emmanuel Okwi na John Bocco waliokosa mabao. Kasi ya Meddie Kagere, Bocco na Okwi iliwapa wakati mgumu mabeki wa Mtibwa, Cassian Ponela na Dickson Daud ambao walikuwa na kazi ya ziada kuokoa hatari langoni mwao.

Dakika ya 30 nusura Mtibwa ifunge bao lakini kiki ya Haruna Chanongo ilitua mikononi mwa kipa Aishi Manula.

Simba ilipata bao la kwanza dakika ya 32 lililofungwa na Bocco alipomalizia vizuri kwa mguu wa kulia mpira wa krosi uliopigwa na Kagere.

Dakika ya 47 Simba ilipata bao la pili lililofungwa na Clatous Chama kwa mguu, baada ya kupata pasi ya Haruna Niyonzima.

Simba: Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein, Erasto Nyoni, Yusuph Mlipili, Jonas Mkude, Clatous Chama, Haruna Niyonzima/Hassani Dilunga, John Bocco/ Mzamiru Yassin, Meddie Kagere/Adam Salamba na Emmanuel Okwi.

Mtibwa: Shaban Kado, Salum Kanoni, Issa Rashid, Cassian Ponela, Dickson Daud, Shaban Nditi, Jafari Kibaya/Saleh Abdallah, Ally Makarani, Riphat Hamis, Salum Kihimbwa/Juma Luizio na Haruna Chanongo/Ismail Aidan.

Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu uliochezwa jana, Kagera Sugar ilichapwa mabao 3-1 dhidi ya Stand United.

Katika hatua nyingine, mshambuliaji nyota wa Yanga, Heritier Makambo ametia saini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na klabu ya Horoya ya Guinea. Makambo raia wa DR Congo alijiunga na Yanga msimu uliopita na hadi sasa amefunga mabao 16 msimu huu.