http://www.swahilihub.com/image/view/-/5113882/medRes/2342460/-/qjrqngz/-/simba+pic.jpg

 

Simba ilikosea hapa

Na Charles Abel, Mwananchi cabel@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Tuesday, May 14  2019 at  09:54

 

Dar es Salaam. Benchi la ufundi la Simba lina kila sababu ya kuitazama na kuongeza ufanisi katika safu yake ya ushambuliaji, vinginevyo inaweza kuwagharimu katika mechi tano zilizobaki za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Matokeo ya suluhu dhidi ya Azam FC jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, yanatoa ishara isiyo nzuri kwa safu ya ushambuliaji ya Simba hasa kipindi hiki muhimu ambacho vita ya ubingwa imepamba moto.

Ni sare ambayo sio tu imezidi kuichelewesha Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu bali pia ni muendelezo wa safu ya ushambuliaji kutofunga bao ikiwa ni mechi ya pili baada ya kushindwa katika mchezo waliopoteza kwa kulala bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye uwanja huo.

Baada ya kupata ushindi wa taabu dhidi ya Mbeya City, Prisons, JKT Tanzania wa bao 1-0 katika kila mchezo, safu ya ushambuliaji ya Simba ilirudisha matumaini kwa kuibuka na ushindi mnono ilipovaana na Coastal Union iliposhinda 8-1, lakini kutofunga dhidi ya Kagera Sugar na Azam FC, kunaweza kuleta wasiwasi katika kipindi hiki ambacho timu hiyo inapambana kuhakikisha inatwaa ubingwa.

Ikiwa timu pinzani zitafanyia kazi kile kilichofanywa na safu ya ulinzi ya Kagera Sugar na Azam, hali inaweza kuwa ngumu kwa Simba katika mechi tano zinazofuata ambazo inahitajika kupata ushindi katika michezo kitatu tu ili itangaze ubingwa.

Ni mechi iliyokuwa na malengo tofauti kwa timu zote mbili ambapo kwa Simba kama ilivyo wazi wao hesabu walizoingia nazo ni kusaka ushindi ili iweze kujitengenezea mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Ingawa Azam haipo katika mbio za ubingwa, mchezo wa jana ulikuwa ni kwa ajili ya kujiimarisha katika nafasi ya tatu, kulinda heshima lakini pia kumaliza unyonge walionao mbele ya Simba ambao hawajawafunga katika mechi nne mfululizo za Ligi Kuu walizokutana kwa miaka miwili na miezi mitatu.

Timu hizo zote mbili jana ziliingia uwanjani zikionyesha tamaa ya kusaka ushindi na hata namna mpangilio wa vikosi vyao ulivyokuwa, ulionyesha wazi kuwa mpango mkuu ni kushambulia na si kujilinda.

Timu zote mbili zilianza na mfumo wa 4-4-2 huku vikosi vyao vikiwa na kundi kubwa la wachezaji ambao aina ya soka lao ni la kushambulia Azam ikiwa na mawinga asili wawili, washambuliaji wawili na kiungo mmoja mshambuliaji.

Simba ilianza na viungo wanne lakini kati yao watatu ni wa ushambuliaji ikionekana ni mkakati wa kuhakikisha inamiliki zaidi mpira na kutengeneza nafasi.

Upangaji wa vikosi ulishabihiana na kile kilichotokea ndani ya uwanja kwani timu hizo zilicheza soka la kushambuliana kuanzia dakika ya mwanzo ingawa mara kwa mara hali ya uwanja uliokuwa na maji kwenye baadhi ya maeneo ilitibua mipango yao katika kusaka mabao.

Lakini hata hivyo licha ya kumiliki mpira na kushambuliana kwa zamu, washambuliaji wa pande zote mbili walionekana kukosa utulivu na kukosa nafasi kadhaa ambazo wangeweza kuzitumia kuzipatia mabao timu zao.

Miongoni mwa nafasi nzuri ambazo Azam ilipata ni ile ambayo Donald Ngoma aliipoteza dakika ya 29 ambapo akiwa anatazama lango, alipiga shuti lililopaa baada ya kupokea pasi nzuri ya chini kutoka kwa Bruce Kangwa.

Shambulizi hilo la Ngoma lilikuwa kama ni kulipa lile lililofanywa na Simba dakika mbili kabla kupitia kwa Meddie Kagere ambaye alipiga shuti lililodakwa na kipa wa Azam, Razak Abalora baada ya kupokea pasi ya Mohammed Hussein 'Tshabalala'.

Simba: Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein, Yusuph Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei, Clatous Chama, Jonas Mkude, Haruna Niyonzima, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi

Azam: Razak Abalora, Nico Wadada, Bruce Kangwa, Yakub Mohamed, Aggrey Morris, Stephan Kingue, Ramadhan Singano, Frank Domayo, Obrey Chirwa, Donald Ngoma, Joseph Mahundi.