http://www.swahilihub.com/image/view/-/4802814/medRes/2138508/-/qvqpc0/-/mo.jpg

 

Simba kufanya kisomo maalum kwaajili ya Mo

Mohammed Dewji ‘MO’, mwanachama na mwekezaji wa klabu ya Simba aliyetekwa na watu wasiojulikana  

Na THOMAS NG’ITU

Imepakiwa - Friday, October 12  2018 at  12:20

Kwa Muhtasari

Lengo ni kumuomba Mwenyezi Mungu aweze kufanya wepesi kwenye matatizo yaliyompata mlezi na mwekezaji huyo.

 

Dar es Salaam. Uongozi wa Klabu ya Simba umeamua kufanya kisomo leo saa 8 mchana baada ya sala ya Ijumaa makao makuu ya Simba, Msimbazi kwa ajili ya kumuombea mwanachama wao Mohammed Dewji ‘MO’ aliyetekwa na watu wasiojulikana jana alfajiri.

Mo alitekwa jana Alfajiri alipokuwa anaenda kufanya mazoezi katika Gym za Hotel ya Colessum iliyopo, Osyterbay jijini Daresalaam.

Lengo la kisomo hicho kupitia taarifa ya Uongozi wa Simba, kumuomba Mwenyezi Mungu aweze kufanya wepesi kwenye matatizo yaliyompata mlezi na mwekezaji huyo.

MO ametekwa alfajiri ya jana Oktoba 11, katika hoteli ya Colosseum iliyopo Masaki, jijini Dar es salaam.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema idadi ya watu wanaoshikiliwa kwa mahojiano kuhusu tukio la kutekwa kwa MO Dewji, imefikia 12 hadi jana jioni.

Mambosasa alitaja idadi ya wafanyakazi watatu wa hoteli hiyo ndiyo wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

"Kwa sasa wako 12 wakiwamo walinzi wote watano waliopo Kampuni ya G1 inayosimamia ulinzi wa hoteli hiyo, pia kuna security Manager wa hoteli,"alisema Mambosasa.

Aidha, Mambosasa amesema watu hao wataendelea kushikiliwa na Polisi. "Wewe mbona unakimbilia kujua wataachiwa lini?,wapo tunavyoongea hivi wako ndani,"amesema Mambosasa alipoulizwa ni lini wataachiwa.