Simba kufungua kampeni ya mwaka huu Uganda

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Tuesday, January 10  2017 at  20:20

Kwa Mukhtasari

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya Kenya itafungua mwaka 2017 ugenini dhidi ya majirani Uganda mnamo Juni 10.

 

Katika ratiba, ambayo imetangazwa Jumanne na Shirikisho la Raga la Kenya (KRU), mechi hii ya mkondo wa kwanza wa Kombe la Elgon itapigiwa jijini Kampala. Simba ya kocha Jerome Paarwater itacheza tena na Uganda katika mechi ya marudiano jijini Nairobi mnamo Juni 24. 

Mechi hii ya marudiano ya Kombe la Elgon pia itakuwa ya ufunguzi ya Kombe la Afrika. Mwaka 2016, Kenya ilipiga Uganda 48-10 jijini Kampala na kuwika 45-24 jijini Nairobi katika mechi ya marudiano ya Elgon Cup, ambayo pia ilikuwa ya Kombe la Afrika. 

Mataifa sita yatashiriki Kombe la Afrika mwaka 2017 tofauti na miaka iliyopita, ambapo kombe hili lilikutanisha timu nne.

Baada ya kumenyana na Waganda, Kenya itaalika Tunisia na Senegal, ambazo zimepandishwa ngazi kushiriki daraja ya juu ya Kombe la Afrika mwaka 2017. 

Kenya kisha itasafiri Kusini mwa Afrika kukabana koo na Zimbabwe na mabingwa watetezi Namibia katika mechi mbili za mwisho za Kombe la Afrika. Simba huenda ikafunga mwaka tena dhidi ya Hong Kong mwezi Agosti.

Katika orodha ya wapinzani wa Kenya mwaka 2017, Namibia ndiyo inakamata nafasi ya juu katika viwango bora duniani.

Namibia inakamata nambari 20, Hong Kong (27), Zimbabwe (37), Senegal (39), Uganda (43) na Tunisia (48). Kenya inakamata nafasi ya 23 duniani.   

  

Ratiba ya Kenya Simba XV (2017):

Juni 10: Uganda vs. Kenya – Kampala (mkondo wa kwanza wa Kombe la Elgon)

 

Juni 24: Kenya vs. Uganda – Nairobi (Kombe la Afrika na mkondo wa pili wa Kombe la Elgon)

 

Julai 8: Kenya vs. Tunisia – Nairobi (Kombe la Afrika)

 

Julai 15: Kenya vs. Senegal – Nairobi (Kombe la Afrika)

 

Julai 22: Zimbabwe vs. Kenya – Harare (Kombe la Afrika)

 

Julai 29: Namibia v Kenya – Windhoek (Kombe la Afrika)

 

Agosti: Kenya vs. Hong Kong (mazungumzo bado yanaendelea).