http://www.swahilihub.com/image/view/-/5068400/medRes/2310742/-/fdiwa8z/-/ratiba+pic.jpg

 

Simba yapangua tena ratiba

Na Mwanahiba Richard, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, April 12  2019 at  11:49

 

Dar es Salaam. Bodi ya Ligi Tanzania jana Alhamisi ilikutana kupanga upya ratiba ya mechi za Simba hususani mechi 11 za viporo.

Hadi sasa Simba imecheza mechi 22 na kukusanya pointi 57 ikikaa nafasi ya tatu kwenye msimamo ambapo inatanguliwa na Yanga yenye pointi 74, Azam ina pointi 63 ingawa kila mmoja imecheza mechi 30.

Mzunguko wa ligi umefika hatua ya 33 ambapo zimebaki mechi tano ili ligi imalizike na kwa mujibu wa ratiba inatakiwa kufikia ukingoni mwishoni mwa mwezi ujao.

Mwananchi inafahamu kwamba wajumbe wa bodi hiyo jana walikutana na tayari ratiba hiyo imepangwa ambapo itawekwa hadharani baada ya mechi ya marudiano ya Simba na TP Mazembe itakayochezwa kesho Jumamosi, Lubumbashi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto alithibitisha kufanyika kwa kikao hicho na kusema kwamba; “Mabadiliko haya sio makubwa yametokana na mechi iliyoahirishwa ya Simba na JKT Tanzania ambayo haikuchezwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha siku hiyo.

“Hivyo mabadiliko yatahusu mechi za Simba tu ambazo ni za viporo na tutatangaza ratiba hiyo wakimaliza mechi yao ya marudiano,” alisema Mnguto.

Habari za ndani kutoka ndani ya bodi hiyo zinaeleza kwamba kusubiri kutangaza ratiba mpya kunategemea na matokeo ambayo Simba itapata katika mechi ya marudiano dhidi ya TP Mazembe.