http://www.swahilihub.com/image/view/-/4801204/medRes/2138508/-/wewja5z/-/mo.jpg

 

Simba yawataka washabiki wake kutumia muda wao kwa dua na sala ili MO apatikane

Mfanyabiashara na mwekezaji wa klabu ya Simba, MO Dewji  

Na Kelvin Matandiko

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  13:02

Kwa Muhtasari

Jeshi la Polisi linawashikilia wafanyakazi watatu wa hoteli ya Colosseum kwa mahojiano

 

Dar es Salaam. Afisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kwa mara ya mwisho kuonekana kwa mfanyabiashara MO Dewji katika klabu hiyo ilikuwa ni jana saa 3:00 usiku kupitia kikao cha bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo.

Manara ametoa kauli hiyo leo saa 5:30 asubuhi alipokuwa akitoa taarifa rasmi ya uongozi wa klabu hiyo kuhusu tukio la kutekwa kwa mwekezaji huyo wa klabu hiyo.

MO ametekwa alfajiri ya leo Oktoba 11, 2018 katika hoteli ya Colosseum alikokuwa amekwenda kwa ajili ya kufanya mazoezi ya viungo.

Hadi sasa Jeshi la Polisi linawashikilia wafanyakazi watatu wa hoteli hiyo kwa mahojiano huku likiendelea na uchunguzi.

"Nikifungua kwa ufupi asubuhi, lakini bodi ya Wakurugenzi imeona itoe taarifa rasmi baada ya kukutana na familia yake, bodi imewaomba shabiki na wapenzi wote wa Simba kwa upande wao watumie muda huu Kwa dua na sala," amesema Manara.

"Kazi ya kumtafuta na kuhakikisha anapatikana akiwa hai na salama iko chini ya Jeshi la Polisi, tuepuke taarifa za upotoshaji mitandaoni."

Manara amesema tukio hilo limewasikitisha uongozi wa Simba kwani jana usiku walikuwa pamoja naye akiwa mwenye hali ya furaha.

"Lakini leo tunapata taarifa hizo, inatuogopesha sana tukio hilo, naomba tuwaachie Jeshi la Polisi wafanye kazi yao, lakini naomba pia shabiki, wapenzi wa Simba na watanzania kwa ujumla tutulie," amesema Manara.