http://www.swahilihub.com/image/view/-/5144244/medRes/2362982/-/77dcwl/-/simbu+pic.jpg

 

Simbu atwaa medali Marekani

Na Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Tuesday, June 4  2019 at  10:45

 

Dar es Salaam.Kocha wa Alphonce Simbu, Francis John amesema kiwango cha mwanariadha huyo katika riadha kimeanza kuimarika.

Kauli ya Francis imekuja saa chache baada ya Simbu kutwaa medali ya shaba kwenye mbio za Rock in Roll Half Marathon Marekani.

Simbu ambaye wiki iliyopita aliambulia nafasi ya 14 katika mbio za Bolder Corolado za kilomita 10 nchini humo, jana alitwaa medali hiyo kwenye nusu marathoni (kilomita 21).

"Ameanza kuimarika na kurejesha makali yake," alisema kocha Francis ambaye alibainisha kwamba mwanariadha huyo na mshindi wa medali ya shaba ya dunia, alishiriki mbio za Roll in Roll ili kuimarisha kiwango chake.

Alisema, Simbu bado ana kiwango bora, ingawa katika mbio za Bolder Colorado na zile za Colombia mwaka jana hakufanya vizuri kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi.

Katika mbio za Rock in Roll, Simbu alitumia saa 1:01:34 na kuibuka mshindi wa medali ya shaba akiwa nyuma kwa dakika 1:26 kwa bingwa Bernard Ngeno aliyekimbia kwa saa 1:00:08 huku Cherono Lawrance akimaliza wa pili akitumia saa 1:00:46.

"Zilikuwa mbio zenye ushindani, kila mmoja alichuana kusaka ubingwa, lakini nilipitwa dakika za mwisho na kutwaa medali ya shaba," alisema Simbu kwa kifupi jana.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelim Gidabuday alisema mwanariadha huyo ni miongoni mwa wanariadha watano ambao RT iliwatafutia mbio nchini Marekani ili kuimarisha viwango vyao.

"Amepambana na kuiwakilisha nchi vema, hiyo ni habari njema kwa Tanzania kipindi hiki ambacho tunajiandaa na mashindano ya dunia ya Septemba kule Doha, Qatar ambako Simbu ni miongoni mwa washiriki," alisema Gidabuday.