http://www.swahilihub.com/image/view/-/4928646/medRes/2211554/-/f7viii/-/ole.jpg

 

Solskjaer akoleza moto Man United

Ole Gunnar Solskjaer 

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  09:19

Kwa Muhtasari

Amewataka wachezaji kujenga utamaduni mpya wa kutaka ushindi katika mechi zote

 

London, England. Ole Gunnar Solskjaer, amewataka wachezaji wa Manchester United kuacha mzaha uwanjani, badala yake anataka ushindi.

Kocha huyo amewataka wachezaji kujenga utamaduni mpya wa kutaka ushindi katika mechi zote ambazo Man United itacheza dhidi ya wapinzani.

Alisema wachezaji wanatakiwa kuwa na hasira ya ushindi lengo ni kuipa mafanikio timu hiyo katika mashindano msimu huu.

Kocha huyo wa muda alisema ana timu imara ya ushindi ambayo ina nafasi ya kufanya vyema endapo wachezaji watajituma.

Solskjaer, mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, alisema ana amini atajifunza mengi kupitia mchezo dhidi ya Tottenham Hotspurs.

Kauli ya Solskjaer imekuja muda mfupi, baada ya Man United kupangiwa Arsenal katika mchezo wa Kombe la FA.

Kocha huyo aliyeipeleka Man United Dubai kwa ziara fupi ya mafunzo, alisema anataka wachezaji wanaojituma wenye kiu ya mafanikio.

“Nimebaini kuna muunganiko mzuri wa pamoja. Kimsingi hali ni nzuri, timu imara. Tuna mechi moja au mbili ngumu hilo ni deni,” alisema kocha huyo.

Solskjaer alisema ana matumaini Paul Pogba atakuwa fiti muda mfupi ujao baada ya kuungana na kikosi hicho akitokea katika majeraha.

Mbali na Ligi Kuu, Man United inajiandaa kwa mchezo mgumu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain wa hatua ya 16 utakaochezwa Februari 12.