Sondre Moen wa Norway anyakua taji Fukuoka Marathon

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Sunday, December 3  2017 at  18:42

Kwa Muhtasari

RAIA wa Norway, Sondre Nordstad Moen ameduwaza miamba wa mbio za kilomita 42 Kenya na Ethiopia kwa kunyakua taji la Fukuoka Marathon nchini Japan, Jumapili.

 

Moen, ambaye muda wake bora kabla ya ushindi huu ulikuwa saa 2:10:07, alijiwekea muda bora wa saa 2:05:48, muda ambao pia ni rekodi mpya ya Bara Ulaya.

Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 26 alivunja rekodi ya mzawa wa Kenya, Kaan Kigen Ozbilen ya saa 2:06:10 iliyowekwa mwaka 2016.

Mkenya Bedan Karoki alikuwa amepigiwa upatu kunyakua taji hasa baada ya kumaliza marathon yake ya kwanza katika nafasi ya tatu jijini London nchini Uingereza mwezi Aprili.

Hata hivyo, Moen alichukua uongozi zikisalia kilomita sita na kukata utepe karibu dakika mbili mbele ya mpinzani wake wa karibu Stephen Kiprotich wa Uganda.

Raia huyu wa Norway ni mkimbiaji wa kwanza kutoka Bara Ulaya kushinda taji la Fukuoka Marathon tangu mwaka 2005.   

 

Matokeo (Desemba 3, 2017):

Sondre Nordstad Moen (Norway) saa 2:05:48

Stephen Kiprotich (Uganda) 2:07:10

Suguru Osako (Japan) 2:07:19

Bedan Karoki (Kenya) 2:08:44

Ammanuel Mesel (Eritrea) 2:09:22

Daisuke Uekado (Japan) 2:09:27

Yoshiki Takenouchi (Japan) 2:10:01

Michael Githae (Kenya) 2:10:46

Yuki Kawauchi (Japan) 2:10:53

Takuya Fukatsu (Japan) 2:12:04