Sportpesa yaamini 'Tujiamini' ndiyo suluhu

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  21:23

Kwa Muhtasari

KAMPUNI ya Sportpesa ambayo inadhamini Shirikisho la Soka Nchini (FKF) na Ligi Kuu ya KPL imezindua mpango wa kurejesha hadhi ya michezo nchini kwa kuwahusisha Wakenya na wadau muhimu.

 

Kupitia mradi huo uitwao “Tujiamini”, Sportpesa inataka Wakenya wote wa matabaka mbalimbali kuungana ili waweze kuinua viwango vya michezo tofauti humu na kuimarisha juhudi za ukuzaji wa vipaji vya chipukizi. 

“Kenya imekuwa ikisifika tangu jadi kama nchi iliyofana michezoni, lakini ni jambo la kusikitisha na vile matokeo yake yamekuwa duni tangu miaka michache iliyopita,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa Sportpesa, Ronald Karauri.

Karauri amesema inafaa Wakenya wajiamini ya kwamba yote yawezekana kupitia ushirikiano wa kila mmoja. Alitaka Sportpesa iungane na washikadau wa michezo ili kukuza talanta, kujenga viwanja na kuwezesha michezo kufanyika kwa mazingira yanayostaili.

“Kila Mkenya anatamani kuona timu za taifa za Kenya zikicheza kwenye kombe la dunia, na kushinda mataji ya kimataifa,” akasema Karauri.

Kinara huyo ameitaka Gor Mahia na klabu nyinginezo za KPL kurejesha kumbukumbu za 1987 ambapo magwiji hao wa soka ya humu nchini walitwaa taji la Mandela Cup miaka 30 iliyopita.

Sportpesa imeanza mradi huu wa Tujiamini kwa kuwahusisha wachezaji waliostaafu na ambao waliwahi kuiletea Kenya sifa tele.