Starlets watafika wapi mtanange wa CAF?

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, November 30  2017 at  13:31

Kwa Muhtasari

MAFANIKIO ya Harambee Starlets katika kampeni za soka ya wanawake kwenye mapambano ya kimataifa mwaka huu yameichochea timu hiyo kuteuliwa kuwania taji la Kikosi Bora cha Mwaka kwenye tuzo zitakazotolewa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) mwishoni mwa mwaka huu wa 2017.

 

Itawajuzu Starlets hata hivyo kuupiku ushindani mkali kutoka kwa Banyana Banyana ya Afrika Kusini na Zimbabwe ili kutia kapuni ufalme wa taji hilo.

Banyana Banyana waliwazidi maarifa wenyeji Zimbabwe katika fainali ya Kombe la mataifa kutoka kanda ya Afrika Kusini (COSAFA) mnamo Septemba 2017 japo nao watalazimika kutoana kijasho na Nigeria na chipukizi wa Ghana wasiozidi umri wa miaka 20 (Under-20) ili kutia kibindoni ubingwa huo wa CAF.

Ufanisi wa Starlets katika juhudi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AWCON) nchini Cameroon kabla ya kuwatetemesha wapinzani wenye uzoefu na tajriba pevu katika soka ya Afrika kwenye fainali za COSAFA 2017 ni miongoni mwa wa mambo yaliyochochea CAF kukitambua kikosi hicho.

Mbali na kuiletea Kenya fahari kubwa kwa ufanisi wa kufuzu kwa fainali za AWCON kwa mara ya kwanza katika historia ya kipute hicho, Starlets ilitia fora nchini Zimbabwe ilikoalikwa kushiriki michuano ya COSAFA iliyofanyika mjini Bulawayo. 
Mataifa mengine yaliyoshiriki kivumbi hicho ni pamoja na wenyeji Zimbabwe, Bostwana, Madagascar (Bukini), Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland na Zambia. 
Starlets walifanikiwa kufika katika hatua ya nusu-fainali lakini kwa bahati mbaya wakaondolewa na wenyeji Zimbabwe kwa kufungwa mabao 4-0. 

Starlets waliopangwa katika Kundi B pamoja na Swaziland, Msumbiji na Mauritius katika COSAFA walionyesha ushapavu katika kundi hilo kwa kumaliza wa kwanza kwa alama tisa baada ya kushinda mechi zote. 

Chini ya mkufunzi Richard Kanyi, Kenya ilianza vyema kwa kuifunga Msumbiji kwa mabao 5-2, ikaifunza soka Mauritius kwa mabao 11-0 na hatimaye Swaziland 1-0. 

Kenya ndiyo iliyokuwa timu ya pekee iliyopata ushindi mkubwa na kupata mabao mengi katika michuano hiyo katika hatua ya makundi ikifuatwa na Zambia iliyofanikiwa kupata mabao 14.

Licha ya Starlets kumaliza kampeni za COSAFA katika nafasi ya nne, timu hiyo inazidi kufufua matumaini ya mashabiki wa Kenya katika fani ya soka ya wanawake iliyokuwa imefifia awali. 

Mbali na kutia tabasamu katika nyuso za Wakenya kwa kutesa wapinzani wao katika majukwaa tofauti ya soka ya kimataifa, uhondo, tija na fahari ambayo Starlets wanazidi kuvunia Kenya ni jambo ambalo mashabiki wa soka ya humu nchini wamekuwa wakilikosa kwa miaka mingi kutoka kwa kikosi cha wanaume, Harambee Stars.

Ikumbukwe kwamba kwa mara ya kwanza mnamo 2016, kulikuwa na michuano ya CECAFA kwa upande wa wanawake mjini Jinja nchini Uganda na Starlets walifanikiwa kufika fainali ila wakazidiwa maarifa na Tanzania.