TUK yaanza kuzinduka kwenye ngarambe ya SPS8 PL

Na JOHN KIMWERE

Imepakiwa - Wednesday, May 16  2018 at  11:34

Kwa Muhtasari

Timu ya Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Kenya (TUK) iliilaza Leads United magoli 5-1 na kupanda hatua nne mbele kwenye kipute cha SportPesa Super Eight (SPS8 PL) 2018, katika patashika iliyochezewa uwanjani Lower Kabete.

 

TIMU ya Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Kenya (TUK) iliilaza Leads United magoli 5-1 na kupanda hatua nne mbele kwenye kipute cha SportPesa Super Eight (SPS8 PL) 2018, katika patashika iliyochezewa uwanjani Lower Kabete.

Mashabiki walifuraha uhondo wa gozi hilo huku wachana nyavu wa TUK wakitembeza ubabe wao dhidi ya Leads United inayoshiriki kipute hicho mara ya kwanza baada ya kupandishwa mwaka 2017 kutoka kipute cha Ligi ya Daraja la Kwanza.

Matokeo hayo yaliipatia TUK ushindi wa pili na kuipiga jeki kusonga mbele. Stephen Juma alicheka na wavu mara mbili, nao Mike Ibande, Steve Augo na Jeconiah Uyoga aliyekuwa akichezea Gor Mahia FC kila mmoja akifunga goli moja.  

TUK ilipata ufanisi huo baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo ilipopigwa mabao 4-2 na RYSA kisha kukomolewa magoli 2-0 na Melta Kabiria. 

Leads United ya kocha, Moses Wekesa ambayo wiki moja kabla ya mchezo huo ilipigwa na Makadara Junior League SA mabao 5-0 ilijipatia goli la kufuta machozi kupitia mchezaji wa kupanda na kushuka Washington Vihembo.

''Kwa kweli tulijaribu kadiri ya uwezo kushusha soka safi na tunatarajia kuzinduka karibuni hasa kutokana na kiwango tulichoonyesha katika patashika hiyo,'' kocha wa TUK, Francis Oduor alisema na kuwataka wanasoka wake kujikakamua kufufua umahiri wao walioteremsha katika ngarambe hiyo miaka miwili iliyopita. Kutokana na matokeo hayo, TUK imetua nafasi ya 12 kwa kuzoa alama saba. 

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Tony Okello alitikisa wavu mara mbili na kuisaidia MASA kulaza Team Umeme magoli 2-1 katika mchuano uliyoandaliwa ugani Makongeni. Naye Oscar Mono alijitahidi kwa udi na uvumba dimbani akisaidiana na wenzake na kuipatia bao la kufuta machozi timu yake Team Umeme.  


MATOKEO MENGINE

Kawangware United 2-0 Zamalek FC

Metro Sports 0-1 Jericho Allstars 

RYSA 0-0 MJLSA 

Shauri Moyo Sportif 2-1 NYSA

Shauri Moyo Blue Stars 3-1 Rongai Allstars