http://www.swahilihub.com/image/view/-/4929274/medRes/2220367/-/8a6epy/-/dk+jonas.jpg

 

Tiboroha amrejesha tena Manji

Anayewania Uenyekiti Yanga, Dk Jonas Tiboroha  

Na Waandishi Wetu

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  14:31

Kwa Muhtasari

Tiboroha amewahakikisha Yanga bilionea huyo atarudi Jangwani

 

 

KAMPENI za wagombea wa nafasi ya uongozi ndani ya Yanga zinazidi kushika kasi, ambapo anayewania Uenyekiti, Dk Jonas Tiboroha amemrejesha Yusuf Manji kimtindo klabuni hapo.

Tangu alipojiuzulu Mei mwaka juzi, wanachama wa Yanga wamekuwa wakimuota Manji wakiamini atarejea klabuni, lakini jana Tiboroha amewahakikisha bilionea huyo atarudi Jangwani.

Yanga itarajiwa kufanya uchaguzi mdogo Jumapili, ambapo kampenzi zimeshaanza ramsi na jana Tiboroha alisema Manji ndiye atakayekuwa mwanachama wa kwanza kumuomba awe mwekezaji klabu hapo kutokana na kuwa na mawasiliano naye ya karibu.

“Kumekuwa na upotoshwaji usiokuwa na tija kwa Yanga, eti nina ugomvi na Manji. Sio kweli mara ya mwisho kufanya mazungumzo naye ni mwezi uliopita, ninatambua umuhimu wake Yanga, nitazungumza nae ili aweze kuwekeza.”

Katibu huyo wa zamani wa Yanga, aliyefanya kampeni yake makao makuu ya klabu, alisema ana vipaumbele sita atakavyovitekeleza ndani ya muda mfupi kama wanachama watamchagua kuwa Mwenyekiti.

“Nitajenga na kuimarisha taasisi. Bado klabu yetu tumeiendesha bila misingi imara ya taasisi ambapo, utendaji uliotukuka ndio nguzo katika taasisi.

“Kingine ni kuirudisha Yanga kwa wanachama na mashabiki. Uongozi wetu unadhamiria kwa nguvu zote kurudisha klabu kwa wanachama kwa kuhamasisha ushiriki wa karibu kwenye kujenga na kuimarisha Yanga,” alisema Tiboroha.

Vingine ni kuimarisha matawi nchi nzima, uwekezaji na biashara, mfumo wa kujenga timu imara, kushirikisha washirika na wadau.

IGANGULA NAYE ALIAMSHA

Naye mgombea mwingine wa Uenyekiti, Mbaraka Igangula aliyezindua juzi Jumanne alisema lengo lake ni kuhakikisha klabu hiyo inahamia kwenye mfumo wa soka la kisasa ili wawe na nguvu kiuendeshaji.

“Ndani ya mwaka wangu mmoja nitafanya mabadiliko makubwa ikiwemo maboresho ya jengo letu na kuhakikisha Yanga inakuwa na uwanja wake wa mazoezi.

“Mfumo wa uwekezaji utarahisisha mambo ndani ya klabu yetu, lengo ni kutaka Yanga iwe na nguvu kubwa, pia nitakuwa makini na vyanzo vyetu vyote vya mapato,” alisema.

Mgombea huyo kwenye kampeni zake yupo sambamba na makamu wake Titus Ossoro pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji, Silvester Bernard Haule, Benjamini Mwakasonda, Atanas Kazige, Ramadhan Said (Chalinze).

Igangula amekuja na kauli mbiu ya Umoja na mshikamano kwa maendeleo ya Yanga.