Timbe apata bao la kwanza kwa klabu mpya

Na  GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, June 19  2017 at  08:10

Kwa Mukhtasari

WINGA matata Ayub Timbe kutoka Kenya alipata bao lake la kwanza katika klabu yake mpya ya Beijing Renhe na kuisaidia kupapura Nei Mongol 3-0 mjini Guiyang, Jumamosi.

 

Mshambuliaji wa Ecuador, Jaime Ayovi alitikisa nyavu za Nei Mongol dakika za sita na 75 kabla ya Timbe kugonga msumari wa mwisho dakika ya 88.

Tangu awasili Feb 20, 2017 kwa kandarasi ya miaka miwili kutoka Lierse nchini Ubelgiji, Timbe amechezea Beijing Renhe mechi 11. Dalian Yifang inaongoza ligi hii ya klabu 16 kwa pointi 30.

Inafuatwa pointi sita nyuma na Beijing Renhe. Klabu hizi mbili ziko katika mduara wa kupandishwa kushiriki Ligi Kuu mwaka 2018.

Katika matokeo mengine ya ligi ya kuingia Ligi Kuu, ilikuwa Dalian Yifang 4 Yunnan Lijiang 0, Xinjiang Tiansham 1 Beijing Baxy 2, Qingdao Huanghai 4 Baoding Yingli Yitong 0, Wuhan Zall 3 Dalian Transcend 1, Shijiazhuang 2 Shanghai Shenxin 1, Shenzhen 4 Hangzhou Greentown 0, Zhenjiang Yiteng 0 Meizhou Hakka 1.

Klabu anayochezea mshambuliaji matata Michael Olunga katika Ligi Kuu ya Uchina, Ghizhou Zhicheng ilizabwa 2-0 na viongozi Guangzhou, Jumamosi.

Zhicheng, ambayo haijapata ushindi katika mechi tatu mfululizo, inashikilia nafasi ya tisa katika ligi hii ya klabu 16.