Tusker yasaka nyota wawili watakaojaza pengo la Wanga

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, November 30  2017 at  13:27

Kwa Muhtasari

MABINGWA mara 11 wa KPL, Tusker wanakaribia kujitwalia huduma za wachezaji Saphan Oyugi na Apolo Otieno ambao walikuwa tegemeo kubwa kambini mwa Chemelil Sugar katika kampeni za Ligi Kuu msimu huu wa 2017.

 

Winga mahiri wa Western Stima, Kevin Okoth pia anasakwa usiku na mchana na Tusker ambao wamepania kukifanyia kikosi chao mabadiliko makubwa kwa nia ya kutoa ushindani unaostahili kwa wapinzani wao wakuu katika kampeni za msimu ujao.

Juhudi za Tusker zimechochewa na hatua ya mvamizi wao matata, Allan Wanga kuweka wazi nia ya kujiunga na Free State Stars ya Afrika Kusini licha ya huduma zake kumezewa mate na klabu ya Zesco United ambayo tayari inajivunia huduma za masogora watatu wa Harambee Stars - Jesse Were, David 'Calabar’ Owino na Anthony 'Teddy’ Akumu.

Kwa mujibu wa George Bwana ambaye ni wakala wa Wanga, fowadi huyo wa zamani wa AFC Leopards anawaniwa pakubwa na Free State ambao wamepania kumtia rasmi katika sajili yao mnamo Januari 2018 baada ya mkataba wake na Tusker kutamatika mwishoni mwa Desemba 2017. 

“Free State wamekuwa wakiyamezea mate maarifa ya Wanga kwa kipindi kirefu. Ingawa bado hawajawasilisha maombi katika juhudi za kurasimisha uhamisho wa nyota huyo, kikosi hicho kimepiga hatua kubwa katika mazungumzo yanayolenga kumshawishi Wanga kujiunga nacho,” akasema Bwana.

Free State kwa sasa wananolewa na mkufunzi mzawa wa Ubelgiji, Luc Eymael ambaye alichangia pakubwa kuimarika kwa makali ya Wanga wakati kocha huyo akiwatia makali vijana wa Leopards mnamo 2013.

Kwa upande mwingine, Bwana alikuwa na ushawishi mkubwa katika kufanikisha uhamisho wa Wanga hadi Azam FC ya Tanzania mnamo 2015.

Hata hivyo, itawalazimu Free State kuwapiga kumbo Zesco na Zanaco ambao ni wapinzani wao wakuu katika soka ya Zambia ili kujinasia huduma za Wanga ambaye pia amewahi kuwapigia Petro Atletico ya Angola pamoja na El Merreikh ya Sudan.

Kwa misimu miwili ambapo amevalia jezi za Tusker, Wanga amewashindia waajiri wake hao ubingwa wa Ligi Kuu ya KPL mara moja na pia kuwachochea kutia kapuni Ngao ya GOtv.

Hata hivyo, majeraha yalitishia pakubwa kulemaza makali yake msimu huu ambapo alifanikiwa kucheka na nyavu za wapinzani mara saba pekee.

Mnamo Disemba 2010, Wanga alitia saini mkataba wa miaka miwili na Anh GiaLai ya Vietnam kabla ya kujiunga na Leopards kwa mkopo mnamo 2012. Mnamo 2013, alielekea nchini Oman kufanyiwa majaribio na Al-Nasr kisha akatua jijini Khartoum kuwasakatia, Al- Merreikh mnamo Juni 2014.