Uganda yaongoza jedwali baada ya kulima Kenya kriketi

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, September 11  2017 at  15:29

Kwa Mukhtasari

KENYA ilipata pigo katika juhudi zake za kufuzu kushiriki mashindano ya dunia ya kriketi ya Twenty20 kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 2018 baada ya kulimwa na Uganda kwa wiketi sita mjini Bulawayo nchini Zimbabwe, Jumapili.

 

Uganda inaongoza jedwali la mashindano haya ya wanawake ya Afrika kwa alama sita baada ya kunyamazisha Namibia kwa mizunguko 21, Tanzania kwa wiketi saba na Kenya.

Waganda wanafuatwa na Zimbabwe ambao wamezoa pointi nne kutoka kwa ushindi mbili. Wenyeji Zimbabwe walikung’uta Namibia kwa wiketi nane na kulima Tanzania kwa mizunguko 21. Wazimbabwe watamenyana na Kenya hapo Jumanne.

Kenya lazima ipige Zimbabwe na kisha Namibia hapo Jumatano ili iweze kufika fainali. Itakuwa kibarua kigumu hasa kwa sababu Zimbabwe inapigiwa upatu kushinda mashindano haya ya Afrika.

Kenya imevuna pointi mbili kutoka ushindi wake wa wiketi dhidi ta Tanzania, Ijumaa. Tanzania na Namibia hazijapata pointi yoyote.

Mshindi wa Afrika ataungana na Bangladesh, Ireland, Papua New Guinea, Scotland na Uholanzi moja kwa moja katika mchujo wa mwisho.

Nambari mbili na tatu watakabiliana tena, huku mshindi pia akifuzu. Mashindano ya dunia yataandaliwa West Indies kutoka Novemba 2-25 mwaka 2018.

 

RATIBA

Septemba 12

Kenya na Zimbabwe, Namibia na Tanzania

 

Septemba 13

Kenya na Namibia, Zimbabwe na Uganda

 

Septemba 15

Mechi ya kutafuta nambari nne na nambari tano, mechi ya kutafuta nambari mbili na tatu

 

Septemba 16

Fainali