Uingereza yaonya kuhusu wizi kwenye #LondonMarathon

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Thursday, April 20  2017 at  16:25

Kwa Mukhtasari

IDARA ya polisi nchini Uingereza imeonya mamilioni ya mashabiki wa mbio za London Marathon hapo Jumapili ‘kuchunga mifuko’ yao dhidi ya wadukuzi na wezi.

 

Kulingana na tovuti ya getwestlondon.co.uk, polisi wa Metropolitan pia wameshauri mashabiki jinsi ya kulinda mali yao.

Baadhi ya mbinu za kuweka mali salama ni kuhakikisha vibeti na mifuko inafungwa wakati wowote, mashabiki wabebe mifuko mbele yao, kutumia vibeti ambavyo ni vigumu kufungua na kuficha vibeti katika mifuko isiyoonyesha kuwepo kwa vibeti hivyo.

Pia mashabiki wameshauriwa kuandika nambari ya simu ya familia kwingineko ili mawasiliano yawe rahisi simu ikiibiwa na kutoweka vitu nyuma ya nywele, miongoni mwa mbinu zingine.

Mashindano haya ya kila mwaka yatashuhudia mamia ya maafisa wa polisi wakiweka doria eneo lote la mbio hizo za kilomita 42 kuanzia Blackheath hadi The Mall mjini Westminster. Polisi wa usafiri pia watalinda barabara za chini ya ardhi jijini London.

Mabingwa watetezi Eliud Kipchoge na Jemima Sumgong kutoka Kenya watakosa makala haya ya 37. Kipchoge hakuingia mashindano naye Sumgong amefungiwa nje baada ya kuvunja sheria za kutotumia dawa haramu katika mashindano.

Karibu washiriki 38, 000 wanatarajiwa kutimka katika makala ya mwaka 2017.