Ushuru na Wazito pazuri kuingia KPL 2018

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, November 13  2017 at  15:21

Kwa Muhtasari

USHURU ilizaba Palos 2-0 nayo Wazito ikanyuka Nakuru All Stars 1-0 Novemba 12, huku zikijiweka pazuri kuingia Ligi Kuu ya Soka ya Kenya mwaka 2018.

 

Viongozi Ushuru, ambao walitemwa kutoka Ligi Kuu mwaka 2016, walilemea nambari saba Palos 2-0 kupitia mabao mawili yaliyopatikana katika kipindi cha pili kutokwa kwa Oscar Mbugua na Benson Amianda (penalti).

Vijana wa kocha Ken Kenyatta wamezoa pointi 75 kutoka kwa ushindi 23, sare sita na vichapo vitano katika ligi hii ya klabu 19.

Wazito, ambayo haijawahi kushiriki Ligi Kuu, ilijipa matumaini ya kufanya hivyo baada ya kuzima klabu ya zamani ya Ligi Kuu Nakuru AllStars 1-0. Vijana wa kocha Frank Ouna walitikisa nyavu za Nakuru kupitia Eric Odhiambo dakika ya 68. Wazito wana pointi 74.

KCB, ambayo iliteremshwa hadi Ligi ya Supa ilipomaliza Ligi Kuu ndani ya mduara hatari wa kutemwa mwaka 2015, pia ilisalia katika vita vya kupandishwa daraja baada ya kulima Nairobi Stima 3-1. Wanabenki hawa wamevuna pointi 73. Ushindi wao ulizima kabisa matumaini ya nambari tano Stima kuingia Ligi Kuu. Vihiga United inashikilia nafasi ya nne kwa alama 71. Imepiga mechi 33 nazo Ushuru, Wazito na KCB zimesakata mechi 34.   

 

Matokeo (Novemba 12):

Nakuru All Stars 0-1 Wazito

Palos 0-2 Ushuru

Talanta 2-0 Isibania

KCB 3-1 Nairobi Stima

Kibera Black Stars 1-0 Modern Coast Rangers

Kenya Police 3-1 St Joseph’s Youth

Agro Chemical 0-0 GFE 105

 

Ratiba (Novemba 13):

MOSCA vs. Bidco United (Camp Toyoyo)

Nairobi City Stars vs. AP Bomet (Camp Toyoyo)