http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119530/medRes/2346472/-/bwctmaz/-/vita+pic.jpg

 

Vita kubaki Ligi Kuu kaa la moto

Na Charles Abel,Mwananchi cabel@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  11:22

 

Dar es Salaam.Raundi mbili zilizobaki kabla ya pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara kufungwa zinakabiliwa na ushindani mkali wa timu 12 ambazo hadi sasa hazijajua hatima zao kama zitashuka au zitabaki kwenye mashindano hayo msimu ujao.

African Lyon imeshashuka daraja kwani ina pointi 22 ambazo hazitaweza kufikia pointi za timu nyingine yoyote hata kama itapata ushindi kwenye mechi zake tatu ilizobakiza kwa kuwa Mwadui iliyopo nafasi ya 19 ina pointi 37 ambazo ni 15 zaidi ya zile za Lyon huku timu ambazo zinashuka daraja moja kwa moja zikiwa ni mbili.

Baada ya African Lyon kushuka, inasakwa timu moja ya kuungana nayo moja kwa moja lakini pia timu nyingine mbili ambazo zitamaliza kwenye nafasi ya 17 na 18 katika msimamo wa Ligi Kuu zitakazocheza mechi za mchujo 'play offs' dhidi ya timu mbili za Ligi Daraja la Kwanza.

Tofauti ndogo ya pointi baina ya timu hizo 12 Mwadui FC, JKT Tanzania, Stand United, Ruvu Shooting, Prisons, Alliance, Biashara United, Mbao FC, Kagera Sugar, Mbeya City, Coastal Union na Singida United inasababisha kila timu kufanya hesabu zake kwa umakini ili kujinasua na janga la kushuka daraja.

Mwadui yenye pointi 38 ipo kwenye hatari zaidi ya kuunga na African Lyon kwani kama itapoteza au kutoka sare katika mechi moja kati ya mbili ilizobakiza, itajiweka pabaya zaidi kwa sababu imezidiwa pointi mbili na Biashara United iliyopo nafasi ya 18 hukuwa wakiwa na mechi tatu mkononi.

Kwa upande wa Biashara United licha ya kuwepo nafasi ya 18, inaweza kujinasua kushuka daraja ikiwa itapata ushindi katika mechi zake tatu zinazofuata kwa kuwa itafikisha pointi 49 lakini hali inaweza kuwa mbaya kama itapoteza au kutoka sare na itabidi ilazimike kuombea wapinzani wake wengine wateleze.

Lakini JKT Tanzania yenye pointi 41 kama ilivyo kwa Stand na pia Ruvu Shooting yenye 42, zinaweza kuporomoka ikiwa zitapoteza mechi zao ambazo wamebaki nazo mkononi na ikiwa Biashara United na Mwadui zenyewe zitapata ushindi.

Timu nyingine ambazo bado hazijajihakikishia kubaki ni Kagera Sugar na Prisons zenye 43, Mbao, Coastal na Alliance ambazo zina pointi 44, na Singida United yenye 45 na Mbeya City iliyo na pointi 46 zinaweza nazo kujikuta zinashuka ikiwa zitapoteza mechi zao zilizobaki na kisha wapinzani wao kwenye vita ya kushuka wakashinda.

Mbaya zaidi ni kwamba zipo timu zilizobakiza mechi mbili na nyingine tatu jambo ambalo linaonyesha kwa jinsi gani kila moja itajipanga kupambana ili kuhakikisha hairuhusu nyingine kuipiku.

Beki wa JKT Tanzania, Charles Edward alisema timu yake ina nafasi ya kubaki na wamejipanga kuhakikisha hilo linatimia. "Ligi ni kama mbio ndefu, hupaswi kukata tamaa. Tutapambana hadi mwisho nina imani tutabaki," alisema Edward.

Kocha wa Stand United, Athumani Bilali alisema ligi ni ngumu ila watahakikisha wanabaki."Kama unavyoona hatujapishana kwa tofauti kubwa ya pointi hivyo kama ukishinda mechi, unasogea juu kwa nafasi nyingi na kuwashusha wengine. Jambo la muhimu ni kutotazama wengine wanafanya nini bali ni kushinda mechi zako," alisema Bilali.

Ofisa Habari wa Alliance, Jackson Mwafulango alisema matokeo waliyopata dhidi ya Biashara United ugenini yanawapa matumaini ya kubaki.

"Tulikuwa kwenye hali mbaya lakini kwa kushinda mechi ngumu dhidi ya Biashara, United naamini hata kisaikolojia tuko sawa," alitamba Mwafulango.