http://www.swahilihub.com/image/view/-/5068388/medRes/2310808/-/vkebcoz/-/simba+pic.jpg

 

Wachezaji Simba wala kiapo Dar

Na Thobias Sebastian, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, April 12  2019 at  11:45

 

Dar es Salaam. Wakati Simba imeondoka nchini leo asubuhi kwenda DR Congo, wachezaji wa timu hiyo wameahidi kucheza kufa au kupona ili kupata matokeo mazuri katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya TP Mazembe.

Simba na TP Mazembe zinatarajiwa kucheza mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Katika mechi ya awali iliyochezwa Dar es Salaam, timu hizo zilitoka suluhu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam, wachezaji wa timu hiyo walisema wanakwenda DR Congo wakiwa na morali ya kushinda.

Beki wa kati Erasto Nyoni alisema mechi itakuwa ngumu tofauti na mchezo wa kwanza kulingana na matokeo yalivyokuwa kwa kuwa kila timu itataka matokeo mazuri ili kusonga mbele.

Beki huyo alisema ingawa TP Mazembe itakuwa na faida ya kucheza kwenye uwanja wake wa nyumbani, lakini wachezaji wana ari ya ushindani kama ilivyokuwa katika mechi ya awali kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Nyoni alisema benchi la ufundi limewapa mafunzo na mbinu za kutosha katika maandalizi na miongoni mwa mambo aliyokuwa akifanyia kazi kocha Patrick Aussems ni kupiga penalti.

Katika mafunzo ya jana, Aussems alisimamia upigaji wa penalti ikiwa ni maandalizi ya mchezo endapo timu hizo zitafikia hatua ya kupigiana penalti.

“Tumefanya maandalizi ya kutosha na mbinu nyingi ambazo tunakwenda kuzitumia katika mechi yetu ya marudiano huku tukiamini tunaweza kupata matokeo mazuri,” alisema Nyoni.

Nahodha wa Simba John Bocco alisema kwanza anatambua mchezo wa marudiano utakuwa mgumu kwa kuwa wanakwenda kucheza na timu kubwa na ngumu na mabingwa hapa Afrika.

Bocco alisema maandalizi ambayo wamefanya ni mazuri na wamepewa mbinu za kutosha kutoka benchi la ufundi, lakini kila mchezaji ana morali ya kushinda mechi hiyo.

Kiungo mkabaji Mghana James Kotei alisema wanakwenda kucheza mechi ngumu lakini lazima wapate matokeo mazuri katika michezo huo.

Beki wa kulia Zana Coulibaly alisema TP Mazembe ni timu kubwa ina wachezaji wazoefu wa mashindano ya kimataifa, lakini watapambana kupata ushindi katika mchezo huo.

Simba inatarajiwa kuondoka leo Ijumaa asubuhi kwa ndege ya kukodi ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 30 kwenda DR Congo