Wachezaji bora KPL kutuzwa Januari 2018

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, November 30  2017 at  13:39

Kwa Muhtasari

WASHINDI wa vitengo mbalimbali katika tuzo za kila mwaka za kampuni ya KPL ambayo huendesha Ligi Kuu ya humu nchini watajulikana mnamo Januari 2018.

 

Ingawa tarehe kamili ya kutolewa kwa tuzo hizo za Wachezaji Bora wa Mwaka (FOYA) haijajulikana, waratibu wa hafla hiyo wamesisitiza kwamba kusogezwa kwa hafla hiyo kulichochewa na maandalizi ya makala ya 39 ya fainali za CECAFA humu nchini.

Fainali hizo za mataifa 12 zitanogeshwa katika viwanja vya Bukhungu Kakamega na Kenyatta Machakos kati ya Desemba 3-17, 2017.

Mwaka wa 2016, hafla ya tuzo za FOYA ambazo hutolewa na KPL kwa ushirikiano na Chama cha Wanahabari wa Michezo nchini (SJAK) na kampuni ya SportPesa ambao ni wadhamini wa Ligi Kuu ya Kenya ilifanyika mnamo Desemba 13 katika hoteli ya Safari Park, Nairobi.

Tuzo hizo hupania kutoa jukwaa na fursa ya kutambuliwa na kutuzwa kwa jitihada za wachezaji waliotia fora zaidi na kutambisha vikosi vyao katika kampeni za KPL kwenye msimu uliokamilika.

Shughuli ya kuteuliwa kwa wawaniaji na kutolewa kwa tuzo za mwisho wa msimu huu wa KPL zitaelekezewa macho zaidi baada ya mashabiki kukosoa pakubwa mfumo uliotumiwa na waandalizi wa tuzo hizo mwaka wa 2016. 

KIPA BORA 
Patrick Matasi (Posta Rangers) ndiye aliyetwaa taji la mlinda-lango bora wa 2016 baada ya kufungwa jumla ya mabao 15 pekee na kuiwezesha Rangers kumaliza kampeni za ligi katika nafasi ya nne kwa alama 45. Aliwashinda David Okello (Tusker FC), James Saruni (Ulinzi Stars), Michael Wanyika (Kakamega Homeboyz) na bingwa wa 2015, Boniface Oluoch (Gor Mahia).
 
DIFENDA BORA 
Joackins Atudo wa Rangers alinyanyua taji hilo licha ya ushindani mkubwa kutoka kwa masogora George Owino (Mathare United), Noah Abich (Sofapaka), Musa Mohammed (Gor Mahia) na James Situma (Tusker FC). Difenda mzawa wa Burundi, Karim Nizigiyimana alitawazwa Beki Bora wa 2015 akivalia jezi za Gor Mahia.

KIUNGO BORA 
Ingawa mashabiki walimpigia upatu Humphrey Mieno (Tusker) kunyanyua ubingwa wa taji hilo, alikuwa ni Kenneth Muguna wa Western Stima ndiye aliyetawazwa mshindi. Ushawishi wa Muguna ulihisiwa pakubwa katika mechi za msimu jana, akichangia ufanisi wa Stima kufunga orodha ya sita-bora kwa alama 44 chini ya kocha Henry Omino.

MCHEZAJI MPYA BORA 
Uwezo alionao tineja Eric 'Marcelo' Ouma haukupingika kabisa katika safari ya kuwania ubingwa wa taji hilo. Kwa pamoja na Mrwanda Jacques Tuyisenge ambaye pia aliteuliwa kuwania ubingwa huo, Ouma aliwachochea Gor Mahia kushikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 54, saba pekee nyuma ya Tusker.
 
MCHEZAJI BORA 
Muguna aliwashinda Eric Ouma (Gor Mahia), John Makwatta (Ulinzi Stars), David Okello (Tusker FC) na Humphrey Mieno (Tusker FC) na kuondoka na Sh1 milioni ambazo mshindi wa taji hilo alipokezwa.