http://www.swahilihub.com/image/view/-/4844092/medRes/1986825/-/1hugsa/-/kaheza.jpg

 

Wadau waibuka Kaheza kutemwa Simba

Marcel Kaheza 

Na Waandishi Wetu

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  12:57

Kwa Muhtasari

Mchezaji anapaswa kuwa na meneja wa uhakika ambaye atamuongoza katika mkataba

 

Dar es Salaam. Unakumbuka majina ya washambuliaji wawili hodari waliong’ara msimu uliopita, Marcel Kaheza na Mohammed Rashid waliotamba katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kaheza aliyetamba Majimaji ya Songea na Rashid Prisons ya Mbeya, walijulikana baada ya kuongoza kwa kufunga mabao katika timu zao kabla ya kusajiliwa na Simba.

Wakati Kaheza akifunga mabao 12, Rashid aliweka wavuni 10 na kuziweka katika ramani timu zao msimu uliopita.

Idadi kubwa ya wadau wa soka waliamini wachezaji hao waliokuwa wakiinukia vyema, wangeendeleza makali yao msimu huu, lakini hali imekuwa tofauti.

"Mchezji ajipime, apime kiwango chake kabla ya kufikiria kusajiliwa na Simba au Yanga ikiwezekana abaki kwenye timu yake inayompa nafasi ya kucheza," alisema Kocha  Mohammed ‘Adolf’ Rishard.

Alisema Simba iko sahihi kuwatema Kaheza na Rashid kwa kuwa falsafa ya klabu kubwa duniani ni matokeo, hivyo haiwezi kulea wachezaji wanaosugua benchi.

"Kukosa kujiamini ndicho kinachotokea kwa wachezaji wengi, mchezaji anaweza kuwa staa kwenye timu ndogo anaposajiliwa Simba au Yanga anakutana na mastaa wengine, anapoteza kujiamini,” alisema nyota wa zamani wa Yanga.

Mchambuzi wa Soka, Ally Mayay alisema Kaheza na Rashid ni wachezaji vijana ambao walipaswa kuwa na usimamizi bora kabla ya kujiunga na Simba.

"Kwa vijana kama hao kipaumbele hakikupaswa kuwa fedha, walipaswa kuangalia kipaji kwanza, ni bora ubaki kwenye timu inakulipa mshahara kidogo, lakini inakupa nafasi ya kukuza na kuendeleza kipaji chako, kuliko mshahara mkubwa halafu unaua kipaji," alisema Mayay.

Nahodha huyo wa zamani wa Yanga, alisema mchezaji anapaswa kuwa na meneja wa uhakika ambaye atamuongoza katika mkataba unaozungumzia kipengele cha kucheza kwa asilimia 50 au 100 kabla ya kujiunga na klabu mpya.