Wakenya kutoana jasho Shanghai Marathon

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Sunday, November 12  2017 at  14:47

Kwa Muhtasari

WAKIMBIAJI Margaret Agai, Rael Kiyara, Peter Kimeli na Mariko Kiplagat kutoka Kenya watawania taji la Shanghai Marathon hapo Novemba 12, 2017.

 

Bingwa wa Paris Marathon nchini Ufaransa mwaka 2013 Kimeli na bingwa wa Beijing Marathon nchini Uchina mwaka 2015 Kiplagat wana kibarua kigumu kurejesha taji la wanaume ambalo Kenya ilishinda mara ya mwisho kupitia Paul Lonyangata mwaka 2015.

Wakimbiaji wanaotarajiwa kubabaisha Wakenya katika kitengo cha wanaume ni raia wa Afrika Kusini Stephen Mokoka, ambaye alishinda mataji ya mwaka 2013, 2014 na 2016 na Waethiopia Gashaw Asfaw, Dino Sefir, Endeshaw Negesse na Abayneh Ayele.

Agai na Kiyara, ambaye alishinda Shanghai Marathon mwaka 2015, watakabiliana na bingwa mtetezi Roza Dereje na bingwa wa mwaka 2014 Tigist Tufa wote kutoka Ethiopia.