http://www.swahilihub.com/image/view/-/4705318/medRes/2074211/-/u7b2iv/-/bett.jpg

 

Wakenya wamlilia Bett huku Uturuki ikipumulia mashine kwa ajili ya kifo chake

Aliyekuwa bingwa wa dunia wa kuruka viunzi mita 400, Nicholas Bett  

Na Waandishi Wetu

Imepakiwa - Thursday, August 9  2018 at  15:15

Kwa Muhtasari

Aliiwakilisha vyema Kenya katika riadha kwa kutwaa medali

 

Nairobi, Kenya. Jana taifa la Kenya na jamii ya wanariadha duniani waliamkia habari za tanzia kufuatia kifo cha aliyekuwa bingwa wa dunia wa kuruka viunzi mita 400 Nicholas Bett.

Bett aliaga dunia baada kupata ajali mbaya kwenye  barabara kuu ya Eldoret-Kapsabet eneo la Sochoi kaunti ya Nandi. Mwanariadha huyo alikumbana na mauti wakati akitoka jijini Nairobi, siku moja baada ya kushiriki mbio za wanariadha wachanga Barani Afrika zilizokamilika majuzi Asaba nchini Nigeria.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa polisi kaunti ya Nandi Bw Patrick Wambani alisema kwamba Bett ndiye alikuwa akiendesha gari lake aina ya Toyota Prado SUV, ambapo alirushwa nje baada ya gurudumu la nyuma la upande wa kushoto kutoka.

Gari hilo liligonga tuta la barabara na kupoteza mwelekeo. Afisa huyo alisema lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi na baada ya kupoteza mwelekeo likaingia kwenye mtaro.

Kwa hakika mauko ya nyota huyo ni pigo kuu kwa dunia ikikumbukwa kwamba alikuwa mwanariadha wa kwanza Kenya kushinda nishani ya dhahabu mita 400 kwa kuruka viunzi katika mashindano ya makala ya 15 ya International Association of Athletics Federation (IAAF) Beijing, China 2015.

Rais wa Kenya, Bw Uhuru Kenyatta akimuomboleza Bett alimtaja kama mwanariadha aliyezolea taifa lake sifa chungu nzima katika nyanja za michezo. "Ni fedheha na mfadhaiko kupoteza kiungo muhimu wa Kenya kama Nicholas Bett. Alizolea taifa hili shime kuu katika riadha duniani, ninatuma salamu zangu za rambirambi na pole kwa familia yake," Rais Kenyatta aliyasema hayo kupitia kitengo chake cha habari na mawasiliano (PSCU).

Naibu wa Rais William Ruto alieleza masikitiko yake kwa kifo cha Bett, akimmiminia sifa tele hasa kwa kuzolea Kenya nishani mbalimbali, sawa na Waziri wa Michezo Richard Achesa. Muungano wa kimataifa wa wanariadha na ule wa Kenya, viongozi mbalimbali, na wanariadha wenza pia walieleza kuhuzunishwa kwao na mauko ya mwanariadha huyo.

Familia ya Bett ni mojawapo ya iliyojaaliwa kwa kipaji cha uanariadha. Baba yake Joseph Boit ambaye ni mwenyekiti wa muungano wa wanariadha tawi la kaunti ya Uasin-Gishu na kaka yake Haron Koech, mwanariadha wa mita 400 na kapteni wa kikosi kilichokuwa Asaba, Jumatano ya mkasa huo walikuwa na wakati mgumu kuafikiana na hali iliyowafika.

Mauti yake si pigo kwa familia, taifa la Kenya, jamii ya wanariadha duniani pekee, ila kwa nchi ya Uturuki. Bett ambaye alikuwa afisa wa polisi, alikuwa ametia saini mkataba na klabu moja nchini humo kuiwakilisha katika kushiriki mashindano ya riadha.

Imebainika kuwa amekuwa akifanya kazi na klabu ya Fenerbahce Istanbul iliyoko Uturuki kwa muda wa miezi saba sasa. Ingawa maelezo ya mkataba huo hayajawekwa wazi, Bett alikuwa awakilishe klabu hiyo katika mashindano mbalimbali ya klabu za riadha za mita 400 za kuruka viunzi.

Katika mashindano ya IAAF Beijing, China 2015 nyota huyo alivunja rekodi ya dunia kwa kwa kuruka viunzi mita 400 na kuweka rekodi mpya ya sekunde 47.79. Vilevile, ameshinda nishani mbili za shaba katika mashindano ya wanariadha wachanga Barani Afrika.

Bett alishiriki mashindano ya kwanza ya kitaifa mwaka 2010, mita 400 kuruka viunzi ambapo alitimka kwa muda wa sekunde 50.39. Aidha, hatua hiyo ilimfungulia awamu kushiriki mashindano mbalimbali ya riadha kitaifa.

Mnamo 2014, aliwakilisha Kenya katika riadha za Jumuiya ya Madola na mashindano ya wanariadha wachanga Barani Afrika, mtawalia. Alianza kushiriki mashindano ya kimataifa 2015. Bett alizaliwa Januari 27, 1990 na kuaga dunia Agosti 8, 2018.