Wakenya washinda mamilioni Singapore Marathon

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Sunday, December 3  2017 at  18:32

Kwa Muhtasari

WAKENYA Cosmas Kimutai na Pamela Rotich wamejizolea Sh5, 151,500 kila mmoja baada ya kutwaa mataji ya mbio za Singapore Marathon, Jumapili.

 

Kimutai na Rotich wameshinda mataji kwa saa 2:22:48 na 2:38:31, mtawalia.

Kimutai, ambaye alidumisha rekodi ya Kenya katika mbio hizi katika kitengo cha wanaume hadi miaka 16, alifuatiwa na somo wake Justus Kimutai (2:23:07) naye Paul Matheka akafunga tatu-bora (2:23:25).

Justus alitia mfukoni Sh2, 060,600 naye Matheka akazawadiwa Sh1, 030,300 katika mashindano haya yanayodhaminiwa na benki ya Standard Chartered.

Nafasi tatu za kwanza katika kitengo cha wanawake pia zimenyakualiwa na Wakenya ambapo Rotich alifuatwa na bingwa wa mwaka 2016 Rebecca Chesir (2:38:48) na Peninah Arusei (2:39:07).

Makala haya ya 16 yamevutia wakimbiaji 48, 400 kutoka mataifa 126.

Rekodi za mbio za Singapore Marathon zilinashikiliwa na Wakenya Luke Kibet (2:11:25) na Salina Kosgei (2:31:55) zilizowekwa mwaka 2009 na 2006, mtawalia.