Wakenya watwaa ubingwa Seoul Marathon

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, March 20   2017 at  20:45

Kwa Mukhtasari

Kenya ilitikisa katika mbio za Seoul Marathon nchini Korea Kusini kupitia wakimbiaji Amos Kipruto na Margaret Agai, Jumapili.

 

Kipruto aliongoza wanaume kutoka Kenya katika kunyakua nafasi 10 za kwanza. Alishinda umbali huo wa kilomita 42 kwa saa 2:05:54

Kipruto alifuatwa na Felix Kipchirchir (2:06:03), Mark Korir (2:06:05), Norbert Kipkoech (2:06:07), bingwa wa mwaka 2012, 2015 na 2016 Wilson Loyanae (2:06:27), Jacob Kibet (2:07:33), Victor Kipchirchir (2:08:52), Felix Kipchirchir (2:09:56), Martin Kiprugut (2:10:43) na Eliud Karioki (2:13:34).

Agai alishinda kitengo cha wanawake kwa saa 2:25:52 akifuatwa na Muethiopia Ashete Bekere (2:25:57) na Mkenya Mercy Kibarus (2:26:52). Mkenya Priscah Jepleting alimaliza katika nafasi ya tano kwa saa 2:28:29

Mara ya mwisho Kenya ilikuwa imefagia mataji ya wanaume na wanawake ya Seoul Marathon ni mwaka 2013 kupitia Franklin Chepkwony na Flomena Chepchirchir.

Ushindi wa Agai ulimaliza utawala wa miaka miwili wa Ethiopia katika kitengo cha kinadada. Kabla ya Agai, Helah Kiprop ndiye alikuwa mwanamke wa mwisho kutoka Kenya kushinda taji la Seoul Marathon mwaka 2014.