Watford, Liverpool zatoka sare

Na GEOFFREY ANENE na MASHIRIKA

Imepakiwa - Saturday, August 12   2017 at  18:42

Kwa Mukhtasari

Watford ilipiga Liverpool breki katika sare ya 3-3 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza mjini Watford, Jumamosi.

 

WATFORD ilipiga Liverpool breki katika sare ya 3-3 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza mjini Watford, Jumamosi.

Wenyeji Watford, ambao walikuwa wamelimwa 2-0, 6-1 na 1-0 na Liverpool katika mechi tatu zilizopita, walianza vyema uwanjani Vicarage Road.
Walipata bao la ufunguzi kupitia kichwa cha mvamizi Stefano Okaka dakika ya nane.

Mwitaliano huyu aliruka vyema baada ya beki wa Ugiriki, Jose Holebas kupiga kona nzuri.

Mshambuliaji wa Senegal, Sadio Mane alisawazisha 1-1 dakika ya 29 baada ya kumegewa pasi safi na kiungo kutoka Ujerumani, Emre Can.

Kiungo Abdoulaye Doucoure kutoka Ufaransa alirejesha Watford mbele 2-1 dakika ya 32 kupitia kombora kali. Liverpool ilikosa nafasi mbili nzuri kutoka kwa Mohamed Salah na Sadio Mane dakika za mwisho mwisho za kipindi cha kwanza.

Salah alipata nafasi nyingine nzuri dakika ya nne ya kipindi cha pili kabla ya kipa wa Watford, Heurelho Gomes kusababisha penalti dakika ya 54, ambayo Mbrazil mwenzake Roberto Firmino aliifunga kwa ustadi na kufanya mambo kuwa 2-2.

Mmisri Salah aliipa Liverpool uongozi dakika ya 57 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Firmino.

Liverpool ilipata nafasi tano nzuri kutoka kwa Alberto Moreno, Joel Matip, Dejan Lovren na Mane, lakini haikuzitumia vyema. Miguel Angel Cabrera aliipokonya Liverpool ushindi katika muda wa ziada kupitia kichwa chake.