http://www.swahilihub.com/image/view/-/5152642/medRes/2368449/-/ovquw6z/-/waziri+pic.jpg

 

Waziri akerwa ubovu Sheikh Amri Abeid

Na Bertha Ismail, Mwananchi

Imepakiwa - Tuesday, June 11  2019 at  10:56

 

Arusha. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harison Mwakyembe amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchukua hatua kuhusu ubovu wa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Akizungumza jana, Dk Mwakyembe alisema uwanja huo ni mbovu na  haufai kwa matumizi kwa kuwa unaweza kuhatarisha maisha ya wachezaji.

Waziri huyo amelitaka shirikisho hilo kuchukua hatua kwa watendaji wa uwanja huo kuhakikisha unafanyiwa maboresho, vinginevyo hautatumika.

Alisema hakuna timu ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayokubali kutumia uwanja huo kwa mechi zake kwa kuwa hauna sifa stahiki kwa matumizi ya binadamu.

Dk Mwakyembe alisema amefikia kutoa uamuzi huo baada ya agizo lake alilotoa kutotekelezwa na watendaji wa uwanja huo unaomilikiwa na Chama cha Mapinduzi.

“Nilikuja nikakuta uwanja umefungwa unafanyiwa maboresho madogo nikawashauri wachimbue nyasi maana zimekuwa magogo na zinaumiza ili kusaidia mchwa wanaotengeneza vichuguu kutoweka lakini pia kuziba mashimo

 “Nashangaa nimerudi tena hapa nimekuta uwanja unaotumika uko vile vile umejaa mashimo hasa eneo la goli sasa niwaambie wamiliki wa uwanja huu kama hamuwezi kuufanyia maboresho tutahamishia mechi uwanja wa kisasa wa Dodoma,” alisema Dk Mwakyembe.

Dk Mwakyembe alisema Serikali haitakuwa tayari kuona viwanja vibovu vikizalisha idadi kubwa ya wachezaji majeruhi wakiwemo wa timu za Taifa.

Kipa wa Yanga Ramadhani Kabwili aliwahi kuumia katika mechi dhidi ya African Lyon, baada ya kutua kwenye shimo aliporuka kuokoa mpira na kulazimika kukaa nje kwa muda baada ya kupata maumivu ya nyonga.

Hata hivyo. Dk Mwakyembe alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka kujenga shule ya michezo ambayo itakuwa na uwanja wa kisasa utakaotumika kwa michezo yote.