Waziri wa Afya afariki akishiriki mbio za Marathon

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, October 9  2017 at  17:51

Kwa Muhtasari

WAZIRI wa Afya nchini Tunisia, Slim Chaker, ameaga dunia akishiriki mbio za marathon ya kuchangisha fedha za kusaidia katika vita dhidi ya ugonjwa wa saratani nchini humo.

 

Shirika la habari la BBC limesema Jumatatu kuwa waziri huyu alipata mshtuko wa moyo akishiriki mbio hizo za kilomita 42.

Kulingana na shirikia hilo, Chaker, 56, alianza kuwa mgonjwa alipokamilisha mita 500 za kwanza na kukata roho katika hospitali moja ya kijeshi.

Waziri Mkuu wa Tunisia, Youssef Chahed alisema kuwa amepoteza “ndugu na rafiki”, ambaye alipoteza maisha akifanya kazi muhimu ya kusaidia wenzake.

Marathon yenyewe iliandaliwa katika mji wa Nabeul unaopatikana katika pwani ya Tunisia mnamo Jumapili kuchangisha fedha za kujenga kliniki ya watoto walio na saratani.

Chaker aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya katika mabadiliko ya baraza la mawaziri mwezi Septemba.