Wembe ni ule ule; Malkia Strikers wanyoa Congo

Na  GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, October 9  2017 at  17:49

Kwa Muhtasari

MALKIA Strikers ya Kenya inanusia kuingia nusu-fainali katika mashindano ya voliboli ya Afrika baada ya kupepeta Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa seti 3-0 jijini Yaounde nchini Cameroon, Jumatatu.

 

Warembo wa kocha Japheth Munala waliingia mchuano huu na motisha ya kuzaba Senegal na Nigeria kwa dozi sawa na hiyo katika mechi mbili za ufunguzi za kundi B.

Katika ushindi wa hivi punde, mabingwa hawa mara tisa wa Afrika, Kenya, walinyakua seti mbili za kwanza 25-17 na 25-15 kabla ya kukamilisha kazi 25-14 katika seti ya tatu.

Dhidi ya Senegal hapo Jumapili jioni, Kenya ilianza vyema kwa kushinda seti ya kwanza 25-21. Ilitolewa kijasho chembamba katika seti ya pili ambapo Edith Wisa alizuia makombora matano yaliyoitoa Kenya chini 19-24 na kusawazisha 24-24 kabla ya seti hiyo kumalizika 28-26.

Baada ya kuponea chupuchupu kudondosha seti ya pili, Kenya ilingia seti ya tatu na ukatili zaidi ikishinda seti hiyo 2515. Mercy Moim na Edith Wisa walichangia pointi 15 muhimu kila mmoja dhidi ya Senegal.  

Benchi la kiufundi la Kenya nchini Cameroon pia liko na makocha David Lung’aho, Josp Barasa na nyota wa zamani Dorcas Ndasaba.

Mechi ijayo ya Kenya itakuwa dhidi ya mabingwa mara tatu wa Afrika, Tunisia, hapo Oktoba 10 saa mbili usiku. Kenya ina jumla ya pointi tisa kutoka ushindi tatu za seti 3-0. Tunisia imepangiwa kupiga mechi yake ya pili baadaye Jumatatu dhidi ya Senegal. Watunisia walilima Nigeria 3-1 katika mechi ya ufunguzi.

Misri na wenyeji Cameroon wako katika kundi A. Mabingwa mara tatu Misri walikanyaga mabingwa wa mwaka 2009 Algeria kwa seti 3-0 nao Cameroon wakachapa Botswana 3-0. Cameroon na Algeria watavaana baadaye Jumatatu.

Mashindano haya ni ya kufuzu kushiriki mashindano ya dunia nchini Japan mwaka 2018.