Were aibeba Zesco kuingia Klabu Bingwa Afrika 2018

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Sunday, December 3  2017 at  18:35

Kwa Muhtasari

MKENYA Jesse Were alipachika mabao mawili na kusaidia Zesco United kuingia Klabu Bingwa Afrika mwaka 2018 baada ya kushinda Ligi Kuu ya Zambia kwa kuzima Mufulira Wanderers 4-2 Jumamosi.

 

Katika mchuano huu ambao Zesco ilihitaji ushindi pekee, mshambuliaji huyu alifunga bao la pili na la tatu katika dakika za 25 na 38 baada ya John Ching’andu kuweka Zesco bao 1-0 juu dakika ya kwanza naye Lazarus Kambole akafunga la ushindi dakika ya 82.

Zesco, ambayo ilikuwa pointi moja mbele ya mabingwa watetezi Zanaco katika ya mechi ya mwisho, ilianza mechi vyema. Hata hivyo, ilijipata pabaya baada ya bao la Ching’andu kufutwa na Guily Manziba dakika ya tatu.

Kitumbua cha Zesco kilianza kuingia mchanga pale Manziba alipachika bao la pili dakika ya 20 na kuweka Mufulira mbele 2-1.

Aliwachenga mabeki wanne wa Zesco na kuachilia shuti kali ambalo kipa Jacob Banda hakuweza kuokoa.

Mabingwa hawa wa mwaka 2007, 2008, 2010, 2014 na 2015 hawakufa moyo. Walijizatiti na kusawazisha 2-2 dakika tano baadaye kupitia Were aliyemegewa pasi murwa na Enock Sabamukama. Were aliongeza bao lake la pili dakika ya 38 baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Kambole.

Zesco ilipata nguvu zaidi beki wa Mufulira, Mbelenge Ngulakwey, alipolishwa kadi yake ya pili ya njano dakika ya 58 kabla ya Kambole kugonga msumari wa mwisho. Mabingwa mara tisa Mufulira walitemwa kutoka Ligi Kuu baada ya kichapo hiki.

Mganda Geoffrey Sserunkuma alifungia Buildcon mabao mawili yaliyosaidia klabu hii, ambayo imeajiri Wakenya Clifton Miheso na John Makwata, kushinda Lumwana Radiants 2-1.

Wakenya hawa hawakushiriki mchuano huu wa mwisho. Zesco, ambayo pia ina Wakenya wengine kiungo Anthony Akumu na beki David Owino, ilifika nusu-fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2016.  

 

Matokeo (Desemba 2, 2017):

Zesco United 4-2 Mufulira Wanderers

Lumwana Radiants 1-2 Buildcon

Zanaco 2-0 Forest Rangers

Green Buffaloes 0-1 Green Eagles

Real Nakonde 2-0 Nkwazi

Kabwe Warriors 2-2 Power Dynamos

Nchanga Rangers 2-3 Nakambala Leopards

Nkana 4-0 Konkola Blades