Wilson Kipsang ajitosa kwa siasa

Wilson Kipsang

Mkenya Wilson Kipsang asherehekea baada ya kushinda makala ya 40 ya mbio za Berlin Marathon Septemba 29, 2013. Pia alivunja rekodi ya dunia. Picha/AFP 

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Friday, February 17  2017 at  15:32

Kwa Mukhtasari

Bingwa wa London Marathon mwaka 2012 na 2014, Wilson Kipsang ni mwanariadha wa hivi punde kujitosa katika siasa.

 

BINGWA wa London Marathon mwaka 2012 na 2014, Wilson Kipsang ni mwanariadha wa hivi punde kujitosa katika siasa.

Kipsang, ambaye amewahi pia kushinda mbio za Berlin Marathon na New York City Marathon, alitangaza Februari 16 kuwa atawania ubunge wa Keiyo Kusini katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 8, 2017.

Mbunge wa eneo hilo ni Jackson Kiplagat Kiptanui, ambaye aliingia bunge kupitia chama cha URP.

Ingawa hajatangaza chama atakachotumia, Chama, ambacho kina ufuasi mkubwa wakati huu katika eneo hilo linalopatikana katika kaunti ya Elgeyo Marakwet ni Jubilee Party.

Alinukuliwa Alhamisi na gazeti la Daily Nation akisema yuko tayari kupigania tiketi kuanzia kura za mchujo.

Uvumi kuwa Kipsang’ alikuwa akimezea mate kiti cha ubunge cha Keiyo Kusini ulichipuka mara ya kwanza mapema Desemba mwaka 2016, siku chache tu baada ya bingwa mita 800 wa Olimpiki mwaka 2008 Wilfred Bungei kutangaza atagombea kiti cha ubunge cha Emgwen kinachoshikiliwa na Alexander Kosgey.

Wabunge Wesley Korir (Cherangany) na Elijah Lagat (Chesumei) wanatarajiwa kuwa uwanjani kutetea viti vyao.

Korir ni bingwa wa zamani wa Boston Marathon mwaka 2012 naye Lagat anafahamika sana kwa kushinda Berlin Marathon mwaka 1997 na Boston Marathon mwaka 2000. Kipsang’ atakuwa nchini Japan kupigania taji la Tokyo Marathon mnamo Februari 26.